Basata wazindua Tuzo za Muziki Tanzania (TMA)

Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Dkt. Kedmon Mapana, leo Oktoba 24, 2025, ametangaza rasmi uzinduzi wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA 2024) — Tanzania Music Awards.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Dkt. Mapana alisema kuwa msimu wa Tuzo za Muziki Tanzania (TMA 2024) umeanza rasmi leo, huku mfumo wa kupokea kazi za wasanii kwa ajili ya kushindanishwa katika vipengele mbalimbali ukianza kufanya kazi rasmi.
“Huu ni mwanzo wa safari mpya yenye matumaini, heshima na hamasa kwa wasanii wetu na sekta ya muziki kwa ujumla,”
alisema Dkt. Mapana.
Ameongeza kuwa lengo kuu la tuzo hizo ni kutambua, kuthamini na kuenzi mchango wa wasanii wa muziki nchini Tanzania, pamoja na kuhamasisha ubunifu, umahiri na ushindani chanya katika tasnia ya muziki.
“Tunatoa jukwaa la kipekee la kuonyesha ubunifu, ujuzi na mafanikio ya wasanii wetu katika kukuza utamaduni, burudani na uchumi wa sanaa,”
alisisitiza Dkt. Mapana.
Tuzo za Muziki Tanzania (TMA 2024) zinatarajiwa kufanyika tarehe 13 Desemba 2025, na wasanii wote wanahimizwa kuwasilisha nyimbo zao kwa njia ya mtandao kupitia mfumo maalum ulioundwa kuhakikisha mchakato wa usaili ni wa kisasa, haki na unaoaminika.
🔗 Tuma kazi zako kupitia: https://awards.basata.go.tz






