Benki ya NMB yatoa Milioni 42.5 maonyesho ya Nanenane Simiyu  

Benki ya NMB imetoa Shilingi Milioni 42,500,000 kwa ajili ya kudhamini maonyesho ya Nanenane ya
yatakayofanyika kitaifa Kanda ya Magharibi katika viwanja vya Nyakabindi Mkoani Simiyu kuanzia tarehe 01 hadi
08 Agosti, 2020 kwa kauli mbiu isemayo “Kwa Maendeleo ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi Chagua Viongozi Bora
2020“.

Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi – Sospeter Magesse akimkabidhi mfano wa hundi yenye thamani ya sh. Milioni 42.5 Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu- Festo Kiswaga (kulia), ikiwa ni mchango wa benki hiyo kwa ajili ya Maonyesho ya Nanenane Kitaifa yatakayofanyika viwanja vya Nyakabindi Mkoani humo. (Katikati) ni Katibu Tawala wa Mkoa – Mariam Mmbaga na Meneja wa NMB Tawi la NMB Bariadi – Gabriel Paul

Pamoja na kiasi hicho cha pesa, Benki hiyo imekabidhi T-shirt 300 zitakazotumika kwenye maonyesho hayo, ikiwa
ni moja ya udhamini wake. Huu ni mwaka wa tatu mfululizo Benki ya NMB inadhamini Maonyesho hayo.


Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Magharibi – Sospeter Magesse (kushoto) akimkabidhi Tisheti Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Simiyu – Festo Kiswaga (kulia), kama udhamini wa Benki hiyo katika Maonyesho ya Nanenane Kitaifa yatakayofanyika viwanja vya Nyakabindi Mkoani humo.
 
Akikabidhi mfano wa hundi ya Sh. Mil 42.5 kwa uongozi wa Mkoa wa Simiyu Meneja wa benki hiyo Kanda ya
Magharibi- Sospeter Magesse alisema, Benki ya NMB kusaidia sekta ya kilimo ni fahari kwao kwani kupitia kilimo
benki imekuwa ikifanya biashara kubwa ambayo imechangia kukua kwa sekta hiyo.
 
“Kwa miaka mitatu ambayo maonesho hayo yamefanyika Mkoani Simiyu,tayari NMB tumetoa udhamini wa
zaidi ya Mil 100, hii ni katika kuhakiksha sekta hii inakuwa imara na kuongeza pato la taifa,” alisema Magesse
 
"Katika kuunga mkono juhudi za Rais wetu wa awamu ya tano,Dkt John Magufuli kwa miaka mitano ya awamu ya
tano ya serikali yake,mchango wetu kama benki tumeweza kujenga uchumi imara kupitia kilimo na ufugaji"
Magesse.
 
Aliongeza kuwa ndani ya miaka miwili Benki hiyo imefanikiwa kufungua akaunti 500,000 za wakulima ambapo kwa
Mkoa wa Simiyu jumla za akaunti 86,000 za wakulima wa pamba zimefunguliwa.
 
Meneja huyo alisema kuwa kama Benki kinara nchini itaendelea na iko tayari  kuendeleza uhusiano wenye
manufaa kati yao ,wakulima, wafugaji na wadau wengine wa kilimo ili watumie fursa vizuri zilizopo kwenye soko na
kukuza mitaji ya biashara zao.
 
Akipokea mchango huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo – Antony Mtaka, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi- Festo
Kiswaga  ameishukuru Benki hiyo kwa namna ambavyo wanajitoa kusaidia maendeleo ya wananchi hususani
wakulima ambao ndio chanzo kikuu cha ukuwaji wa uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu ya
kilimo bora kwa wakulima, kuwapatia mikopo na kuwafungulia akaunti wakulima.

Related Articles

Back to top button