Biden: Vifo vya corona vimefika 500,000 Marekani, hii inakatisha tamaa (+ Video)

Rais wa Marekani, Joe Biden amehutubia taifa baada ya kurekodi vifo 500,000 vilivyotokana na virusi vya corona, idadi kubwa zaidi kufikiwa ulimwenguni.

”Kama taifa, hatuwezi kukubali mwisho huu mbaya. Tunapaswa kuepuka kufa ganzi kwa huzuni,” alisema.

Rais na Makamu wa Rais , na wake zao, kisha walikaa kimya nje ya White House wakati wa tukio la kuwasha mshumaa.

Zaidi ya Wamarekani milioni 28.1 wamepata maambukizi ambayo pia ni idadi ya juu zaidi duniani.

”Leo ninawaomba Wamarekani kukumbuka. Kukumbuka wale tuliowapoteza na kuwakumbuka tuliowaacha,”

Rais Biden alisema akiwataka Wamarekani kupambana na Covid-19 kwa pamoja.

Biden ameadhimishaje ?

Bwana Biden aliamuru bendera zote kwenye maeneo ya serikali zishushwe nusu mlingoti kwa siku tano.

Katika ikulu ya White House, alifungua hotuba yake kwa kueleza kuwa idadi ya Wamarekani waliokufa na virusi vya corona ni kubwa zaidi kuliko ilivyokuwa idadi ya vifo vya vita vya kwanza vya dunia, vita vya pili vya dunia , na vita vya Vietnam ukijumuisha kwa pamoja.

“Leo tunaashiria hatua mbaya sana, yenye kuumiza moyo – 500,071 wamekufa,” alisema.

“Mara nyingi tunasikia watu wakielezewa kama Wamarekani wa kawaida,” aliendelea kusema. “Hakuna kitu kama hicho, hakuna kitu cha kawaida juu yao. Watu tuliopoteza walikuwa zaidi ya watu wa kawaida . Walikuza vizazi. Walizaliwa Marekani, walihamia Marekani.”

“Wengi wao walivuta pumzi yao ya mwisho wakiwa peke yao Marekani,” aliendelea.

Familia ikimuomboleza Gregory Blanks, 50, aliyekufa kutokana na maradhi ya corona mwezi Januari huko Texas
Familia ikimuomboleza Gregory Blanks, 50, aliyekufa kutokana na maradhi ya corona mwezi Januari huko Texas

Alieleza mfano wa aliyoyapitia kwa uchungu- mke wake na binti yake walipoteza maisha katika ajali ya gari mwaka 1972 na mmoja wa vijana wake alifariki kwa saratani ya ubongo mwaka 2015.

”Kwangu mimi, kupambana na huzuni na uchungu ni kulitafuta kusudi,” alisema.

Jinsi Bwana Biden anavyoshughulikia janga la Covid-19 ni tofauti na mtangulizi wake Donald Trump, ambaye alikuwa na mashaka kuhusu athari za vieusi na kuwa na msimamo kuwa suala la kuvaa barakoa lilikuwa likifanywa kisiasa na hatua nyingine za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Rais Biden na mkewe ,na makamu wake Harris na mume wake, wakinyamaza kutoa heshima kwa waliokufa na corona
Rais Biden na mkewe ,na makamu wake Harris na mume wake, wakinyamaza kutoa heshima kwa waliokufa na corona

Tarehe 19 mwezi Januari, siku moja kabla ya Bw. Biden kuingia madarakni aliadhimisha kumbukumbu ya vifo vya watu 400,000 nchini humo waliopoteza maisha kutokana na virusi vya corona

Tukio la siku ya Jumatatu, limekuja kwa takribani mwezi mmoja baadae.

Kwingineko jijini Washington , kengele katika kanisa ilipigwa mara 500, kwa ajili ya maelfu ya Wamarekani waliopoteza maisha kutokana na janga hilo.

Kinachotokea Marekani

Idadi ya Wamarekani waliokuwa na virusi vya corona ni karibu mara mbili ya nchi ya pili kuwa na idadi kubwa ya maambukizi- India ( milioni 11) na Brazil ( milioni 10.1). Brazil ni ya pili ulimwenguni kwa kuwa na vifo 244,000 wakati Mexico ya tatu ikiwa na vifo 178,000.

Watu miaka 10 kuanzia sasa watazungumzia kuhusu historia mbaya katika nchi hii, kuwa na idadi kubwa waliokufa kutokana na ugonjwa huu,” mtaalamu wa masuala ya kinga Dkt Anthony Fauci, aliiambia CNN Jumapili.

”Ni namba inayoshtua. Mwaka jana sikuweza kufikiri kuwa watu nusu milioni wanaweza kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo,” alisema Dkt Ashish Jha, kutoka shule ya afya ya Chuo Kikuu cha Brown.

”Tuna uwezo, rasilimali nyingi katika nchi hiiā€¦hili liliweza kuzuilika na halikupaswa kutokea. Na sasa tuko hapa,” aliiambia BBC. ”Na ninafikiri tunapaswa kuangazia namna zote ambazo tulikosea katika kushughulikia suala hili.”

Takribani Wamarekani 90,000 zaidi wanatarajiwa kupoteza maisha kutokana na virusi vya corona ifikapo tarehe 1 mwezi Juni, kwa mujibu wa matarajio ya hivi karibuni kutoka Chuo Kikuu cha Washington, Taasisi ya takwimu za afya na tathimini. (IHME)

Taasisi hiyo inakadiria kuwa mpaka mwishoni mwa mwezi Mei, virusi vitaua Wamarekani 500 kwa siku- idadi ya chini kwa makadirio ya vifo 2,000 kwa sasa.

Idadi ya watu wanaofikishwa hospitalini imepungua kwa siku 40 mfululizo wakati ambapo chanjo karibu milioni 1.6 zikitolewa kwa Wamarekani kila siku.

Lakini wataalamu wana wasiwasi kuhusu idadi ya aina virusi vipya nchini humo, ambavyo vinaweza kusababisha milipuko mipya ya ugonjwa huo.

Bofya hapa chini kumsikiliza Biden.

https://www.instagram.com/tv/CLoGpPkB7no/

Related Articles

Back to top button