Habari

Biteko ataka uzalishaji umeme uongezeke na miundombinu kuendelea kuboreshwa

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dk. Doto Biteko amesema ili wananchi waweze kupata umeme wa uhakika nchini ni lazima uzalishaji wa nishati hiyo uongezeke na miundombinu iendelee kuimarishwa.

Naibu Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Julai 10, 2025 wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya miradi ya kuzalisha umeme kwa gesi asilia katika vituo vya Kinyerezi I, Kinyerezi I Extension na Kinyerezi II.

Amesema licha ya kazi kubwa inayofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) yapo baadhi ya maeneo yalikua na changamoto ya upatikanaji wa umeme lakini mpaka sasa yameendelea kuimarika.

Dk. Biteko amesema baada ya nchi kuwa na uzalishaji umeme wa kutosha hatua ya pili ni kuufikisha kwa wananchi na kwamba ni kweli nchi ina umeme mwingi lakini yapo maeneo bado miundombinu yake hayajafanyiwa matengenezo kwa muda mrefu hivyo lazima yafanyiwe marekebisho makubwa kwa haraka.

“Kwa kweli hapa niwapongeze Tanesco kwa kazi nzuri waliyoifanya kwa kipindi hiki, Dar es Salaaam kuna maeneo ambayo yalikuwa na shida sana ya upatikanaji wa umeme ikiwemo Mbagala, Gongo la Mboto, Kigamboni, kazi kubwa iliyofanyika kwanza ni kuboresha miundombinu tuliyokuwa nayo, tulikuwa na transfoma hapa Kinyerezi ambayo inatuma umeme wa matatizo na ilikuwa MVA 50, tumebadilisha na kuweka transfoma kubwa mbili za MVA 150 moja tayari inafanya kazi na nyingine inakamilishwa, Gongo la Mboto pia  na maeneo mengine yanaendelea na maboresho,” amesema Dk. Biteko na kuongeza

“Mahitaji ya umeme nchini yameongezeka hivyo ni lazima uzalishaji uongezeke na miundombinu hiimarishwe ili tuweze kupata umeme wa uhakika na tuwapatie wananchi nishati hii kwa uhakika,” amesema

Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko amefafanua kuwa ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme unaendana na mahitaji ya ongezeko la watu TANESCO inatarajia kuongeza uzalishaji umeme katika Kituo cha Kinyerezi III kutoka megawati 600 katika mpango wa awali hadi kufika Megawati 1000 mpango wa sasa.

‘’Nataka niseme mbele yenu ndugu zangu, Rais Samia ndio Kinara wa kufanya haya yote yafanikiwe amefanya uwekezaji mkubwa kwenye Sekta ya Nishati na ndio maana kwenye bajeti iliyopita Wizara hii imepata Shilingi Trilioni 2.3 kikubwa anataka wananchi wapate umeme wa uhakika, kiu yake ni kuona tunapeleka umeme kwenye vitongoji vyote nchini’’ amesema Dk. Biteko.

Aidha amesisitiza kuwa hivi sasa Tanzania ina umeme wa kutosha hatua ambayo imechangiwa na kukamilika kwa Miradi mikubwa ya uzalishaji umeme ukiwemo Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP ) ambao pekee unazalisha Megawati 2115.

Hata hivyo Naibu Waziri Mkuu pia ametumia nafasi hiyo kuipongeza Tanesco kwa maboresho makubwa yanayoendelea kufanyika ya kuwahudumia wateja hasa kwa uharaka wao wa kukabiliana na dharula zozote za umeme zinazojitokeza.

‘’Kuna maboresho makubwa yamefanyika katika kuwahudumia wananchi naona jitihada kubwa zinafanyika, mmekuwa na uharaka wa kushughulikia changamoto za umeme lakini pia niwapongeze kwa kuimarisha Kituo cha miito ya simu sasa wananchi wanahudumiwa bila gharama yoyote,’’ amesisitiza Dkt. Biteko.

Katika ziara hiyo Dk. Biteko aliongozana na viongozi mbalimbali akiwemo katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati Felchesmi Mramba, Mkuu wa Wilaya ya Ilala,  Edward Mpogolo na Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents