Bunge laipongeza Simba kuingia robo fainali, Naibu Spika Tulia awataja Yanga (+Video)

BUNGE limeipongeza Klabu ya Simba kwa kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), ikiwa ni siku chache baada ya kuwafunga AS Vita ya DR Congo kwa magoli 4-1 kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

Akitoa pongezi hizo (juzi)  bungeni jijini Dodoma Naibu Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson amesema kuna wabunge yawezekana hawajaelewa uzito wa ushindi huo wa Simba “Ni jambo ambalo sisi kama taifa tunapaswa kuungana kuwatia moyo wachezaji wetu na klabu yetu iendelee kufanya vizuri kwa sababu inapata fursa ya kuitangaza nchi yetu vizuri,” alisema.

Dk.Tulia alisema “Naamini mashabiki wa Yanga wataungana nami katika pongezi hizi kwa klabu ya Simba.”

Kikosi cha Simba kwa sasa ipo jijini Cairo, Misri kujiandaa na mchezo wake wa marudiano dhidi ya wenyeji wao klabu ya Al Ahly utakaopigwa siku ya Ijumaa.

Licha ya Simba kuwa na hamasa na shauku kubwa ya kuwaadabisha Waarabu katika ardhi ya nyumbani kwao siku hiyo lakini haina cha kupoteza hata ikifungwa kwakuwa wameshakata tiketi ya kufuzu hatua ya Robo Fainali huku wakiwa vinara kwa alama ambazo hazitofikiwa na timu yoyote katika kundi lake ambalo hapo awali lilifahamika kama kundi la ‘KIFO’.

Kundi hilo la A, Mnyama Simba amejikusanyia pointi 13 pasipo kupoteza mchezo hata mmoja ‘Unbeaten’, Al Ahly wakishika nafasi ya pili kwa alama nane (8), AS Vita ya tatu na pointi zao nne (4) wakati El Merreikh wakiburuza mkia ‘VIBONDE’ na alama zao mbili (2) walizozipata kwa sare.

Related Articles

Back to top button