Habari

CCM yatangaza mabadiliko ratiba uchukuaji fomu za ubunge, uwakilishi na udiwani

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimetangaza mabadiliko ya mchakato wa ndani wa uteuzi wa wagombea wa nafasi ya ubunge, ujumbe wa Baraza la Wawakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

CCM imesema uchukuaji  na urejeshwaji wa fomu za kuomba kuwania nafasi hizo za uteuzi ndani ya chama sasa utaanza rasmi Juni 28, mwaka huu na kukamilika Julai 2, 2025 saa 10:00 jioni.

Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa usiku wa kuamkia leo na Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi imeeleza kuwa wamebadilisha tarehe hiyo kutoka ile ya awali kufuatia mashauriano waliyoyafanya na wanachama wake, kutafakari na kupima kwa makini ushauri huo na hivyo kuamua kufanya marekebisho juu ya ratiba ya awali ya mchakato huo.

Fomu hizo zitakuwa kwa makatibu wa jumuiya za chama hicho zikiwamo UVCCM, UWT na Wazazi ngazi za mikoa kwa nafasi ya viti maalum vya ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi, nafasi ya Ubunge na Ujumbe wa Baraza la Uwakilishi fomu hizo zitatolewa na Makatibu wa CCM Wilaya.

Ratiba iliyotolewa Aprili 10, 2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amos Makalla ilieleza kuwa uchukuaji na urejeshaji wa fomu ungeanza Mei Mosi hadi 15, 2025.

 

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents