Michezo
Chelsea hawataki utani, hizi ni hasira au??

KATIKA harakati za kupanua uwanja wao, Chelsea imenunua jengo lililokuwa makazi ya wanajeshi wastaafu 100 wa jeshi la Uingereza lililokuwa karibu na uwanja wanaoutumia.

Chelsea imetumia kiasi kisichopungua Pauni 80 milioni (Sh 259 bilion) kununua jengo hilo la Sir Oswald Stoll ambapo mchakato ulianza tangu Oktoba, mwaka jana ikiwa ni katika mpango wao wa kupanua Stamford Bridge. Matajiri hao wa Jiji la London wanataka kutumia Pauni 2 bilioni (Sh 6.4 trillioni) kwa ajili ya maboresho ya uwanja na hadi sasa haijafahamika ikiwa wataendelea kuchezea uwanja huo kwa msimu ujao au wataondoka kupisha maboresho.

Mchakato wa kununua jengo hilo ulikuwa unasuasua kwani wanajeshi wastaafu waliokuwa wakiishi hapo waligoma kuondoka wakieleza kwamba wakitolewa watapelekwa kwenye nyumba za zamani zilizochoka. Lakini, Chelsea iliwahakikishia wote wanaotaka kusalia ndani ya Halmashauri ya Fulham timu itawatafutia maeneo mazuri ya kushi.

Ofisa mtendaji wa kampuni iliyokuwa inasimamia jengo hilo, Will Campbell Wroe alisema wana furaha ya kufanikisha mauzo na nia yao ni njema ikiwa ni kutumia pesa watakazopata kujenga na kuboresha nyumba nyingine za wanajeshi wa zamani, Uingereza imekuwa na utamaduni wa kuwatunza vyema wastaafu wa jeshi.
Imeandikwa na Mbanga B.