Habari

Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia chapokea kompyuta 20 kwaajili ya mafunzo ya tehama

Wafanyakazi wa Tigo, kutoka Nyanda za juu Kusini, wakiwa katika ya pamoja na wahadhiri Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST baada ya makabidhiano ya kompyuta 20 katika chuo hicho zenye thamani ya 48m/- zilizotolewa na Tigo kwaajili ya kuchangia katika masomo ya TEHAMA katika chuo hicho mkoani Mbeya.

Mkurugenzi wa Tigo, Nyanda za juu Kusini, Henry Kinabo(katikati), akikaribishwa katika chumba cha kufundishia kompyuta katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) na Rasi Kampasi ya Rukwa, Dkt. Duncan Mwakipesile(Kushoto) baada ya makabidhiano ya komputa 20 zenye thamani ya 48m/- zilizotolewa na Tigo kwaajili ya kuchangia katika masomo ya TEHAMA katika chuo hicho mkoani Mbeya.

 

Katika juhudi za kuchangia malengo ya Serikali ya kuboresha na kuinua viwango vya elimu katika taasisi za elimu ya juu, kampuni inayoongoza katika maisha ya kidigitali nchini Tanzania, Tigo, leo wamekabidhi kompyuta za mezani 20, zitakazo wanufaisha wanafunzi 4,630 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya(MUST).

Alipokuwa anakabidhi kompyuta hizo katika chuo hicho, Mkurugenzi wa Tigo, Nyanda za juu Kusini, Henry Kinabo alisema: “Tunaamini ya kwamba kompyuta tunazozitoa hapa leo, zitachangia sehemu kubwa katika kubadilisha jinsi wanafunzi wanavyosoma na pia zitaleta nafasi kwao kubuni teknolojia mpya na kuchangia katika ukuaji wa uchumi nchini Tanzania. Tigo ipo mstari wa mbele kwaajili ya kuboresha viwango vya elimu katika vyuo vikuu kwa kuleta nyenzo za kusomea na kuwasaidia wanafunzi na walimu kukuza vipengee muhimu vinavyohitajika katika karne hii ya 21.

Aliendelea kuelezea zaidi kwamba kupitia mchango huo, Tigo imeunga mkono juhudi za Serikali ya Tanzania katika mtazamo wake wa kubadilisha nchi kuwa ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 ambapo TEHAMA ndio chachu ya maendelea hayo.

Mnamo mwaka 2017, Tigo ilichangia kompyuta 47 katika Chuo kikuu cha Dodoma, zilizo wanufaisha wanafunzi takriban 36,150. Mpaka leo jumla ya wanafunzi 40,780 katika vyuo vikuu nchini wamenufaika na msaada wa kompyuta kutoka Tigo kwa kipindi cha miaka miwili sasa.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia(MUST), Profesa Aloys Mvuma, aliipongeza kwa mchango wao kwa kusema, “Ni kupitia ushirikiano huu ndio tutaweza kutoa stadi za kisasa za TEHAMA za kisasa pamoja na maarifa kwa kizazi kijacho cha wataalam, ili nchi iweze kukidhi mahitaji ya taarifa zinazobadilika mara kwa mara na mitindo ya kidigitali katika jamii na uchumi wa dunia.

Rasi wa ndaki ya Sayansi na Elimu za Ufundi, Dkt. John.P.John, aliwashukuru Tigo kwa usaidizi wao mkubwa sana na alisema kompyuta hizo zitasaidia kuboresha kiwango cha elimu mkoani Mbeya.

“Tunawashukuru Tigo kwa kusaidia juhudi za serikali kwa kutoa mchango wa vifaa vya kufundishia masomo ya TEHAMA katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia(MUST). Tunaamini ya kwamba hizi kompyuta zitaboresha jinsi wanafunzi wanavyosoma na pia itaongeza ueledi katika elimu ya kidigitali hapa Chuoni.

 

 

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents