Siasa

CNN yamfukuza mtangazaji wake Chris Cuomo, kumsaidia kaka yake mwanasiasa

Mtangazaji wa Marekani Chris Cuomo amefukuzwa kazi na CNN baada ya kumsaidia kaka yake, gavana wa zamani wa New York Andrew Cuomo, alipokuwa akipambana na madai ya unyanyasaji.

Uamuzi huo ulikuja baada ya CNN kusema kuwa habari za ziada zimeibuka juu ya kiwango cha ushiriki wa Chris Cuomo katika utetezi wa kaka yake mkubwa.

Andrew Cuomo alijiuzulu mnamo Agosti baada ya waendesha mashtaka kusema alikuwa amewanyanyasa wafanyakazi.

Chris Cuomo, mwenye umri wa miaka 51, amesema katika taarifa kwamba amekatishwa tamaa na “sio jinsi ninavyotaka wakati wangu kwenye CNN umalizike”.

Alifanya kazi kwenye mtandao huo tangu 2013 na akawa mmoja wa watangazaji wake wa habari wanaotambulika, hivi karibuni akiongoza matangazo ya CNN ya uchaguzi wa rais wa 2020 wa Marekani.

Taarifa ya CNN ilisema kwamba “kampuni ya sheria inayoheshimika” iliajiriwa kuchunguza juhudi za Chris Cuomo kumsaidia kaka yake mwanasiasa kupambana na madai ya unyanyasaji wa kijinsia.

Lakini wakati mchakato huo ulivyofanyika, “taarifa mpya imefichuka” na kusababisha mtandao huo kusitisha mkataba wake mara moja”.

Chris Cuomo alikuwa tayari amesimamishwa kazi na CNN siku ya Jumanne baada ya kufichuliwa kwa juhudi zake za nyuma ya pazia za kusaidia kusafisha kashfa hiyo.

Wakati huo, mtandao huo ulisema kwamba ingawa “unathamini nafasi ya kipekee [Chris Cuomo] aliyokuwa nayo na kuelewa hitaji lake la kuweka familia kwanza na kazi ya pili”, ushauri aliotoa kwa kaka yake ulikuwa ukiukaji wa maadili ya uandishi wa habari.

Hati zilizotolewa na Mwanasheria Mkuu wa New York Letitia James siku ya Jumatatu zilionesha kwamba Cuomo mdogo aliendelea kushinikiza wafanyikazi wa gavana kumruhusu kuchukua jukumu kubwa katika utetezi wa kaka yake.

“Unahitaji kuniamini,” alituma ujumbe mfupi kwa Melissa DeRosa, katibu wa kaka yake, mwezi Machi, na kuongeza: “Tunafanya makosa ambayo hatuwezi kumudu.”

Pia aliahidi kuwasiliana na vyombo vingine vya habari vya Marekani ili kujaribu na kujua kuhusu madai mengine ambayo yalikuwa yanakuja.

Katika barua pepe ya wafanyakazi , ambayo New York Times iliiona, Rais wa CNN Jeff Zucker alisema: “Inaenda bila kusema kwamba maamuzi haya sio rahisi, na kuna mambo mengi magumu yanayohusika.”

Kufukuzwa kwa nyota huyo kutaibua maswali mazito kuhusu viwango vya uandishi wa habari nchini Marekani.

Mwandishi wa habari wa CNN Brian Stelter alisema kuwa “watazamaji wanahitaji kuwa na uwezo wa kuamini kile wanachosikia hapa kwenye runinga tunapoangazia taarifa nyeti, hata ikiwa inahusisha mwanafamilia wa mfanyakazi mwenzako”.

Familia ya Cuomo kwa muda mrefu imekuwa moja ya wadau wakubwa katika siasa za Marekani.

Andrew Cuomo alichaguliwa kwa awamu tatu mfululizo kama gavana wa New York na baba yao Mario aliongoza jimbo hilo kwa zaidi ya muongo mmoja kati ya 1983 na 1994.

Kabla ya kujiuzulu mnamo Oktoba, Andrew Cuomo alikuwa kiongozi mkuu wa kisiasa, kabla ya uchunguzi uliofanywa na Mwanasheria Mkuu wake kuhitimisha kuwa alikuwa amewanyanyasa kingono na kuwapapasa wanawake 11 wanaomfanyia kazi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents