Habari

DC Babati awatangazia vita wanaohujumu miundombinu TANESCO

Mkuu wa Wilaya ya Babati Lazaro Twange ameahidi kula sahani moja na waharibifu na wanaojihuisha na wizi wa miundombinu ya umeme na miradi ya kimakakati inayoendelea kutekelezwa kwa lengo la kuchochea uchumi katika maeneo ya ndani ya Wilaya hiyo.

Amesema hayo wakati akizungumza na wakazi wa mtaa wa Komoto kata ya bagara mjini Babati kufuatia watu wasiofahamika kufanya uharibifu na kuiba vyuma katika nguzo kubwa za umeme zinazotoka nchini Tanzania mpaka katika nchi jirani ya Kenya na kusababisha hasara kubwa kwa shirika la umeme Tanzania (TANESCO).

Mkuu huyo wa Wilaya amesema Serikali haitakuwa na huruma kwa mtu ama kikundi cha watu wanaojihussisha na vitendo vya uhalifu hasa kwenye miundombinu ambayo inagharimu fedha nyingi za wanyonge.Kwa mujibu wa Mh.Twange mradi huo umegharimu zaidi ya shilingi bilioni 500 za kitanzania.

Mh.Twange amesema Umeme ni nishati muhimu kwa uchumi wa nchi hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuwa mlinzi wa miundombinu hiyo.

Twange ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama,amewaomba watendaji wa wa Serikali ngazi mbalimbali ,wenyeviti wa mitaa na Vijiji kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ili kukomesha vitendo hivyo vinavyorudisha nyuma maendeleo.

Kwa upande wake afisa Usalama wa wa shirika la umeme (TANESCO) mkoa wa Singida Davis Mkwiche ameeleza kuwa nguzo tisa katika wilaya ya Babati zimeharibiwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni wezi ambapo wamekata chuma ndogo zilizowekwa kuzunguka nguzo hizo.

Mradi huo wa kimkakati wa utengezaji wa njia ya kusafirisha umeme wa Kilovoti 400 unaotekelezwa kutoka Tanzania hadi nchini Kenya upo katika hatua za mwisho za kukamilika kabla ya kukabidhiwa kwa Tanesco

Mkwiche amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa watu hao baada ya kuiba vyuma huvitumia kutengeneza mikokoteni ambayo inakokotwa na wanyama,mikuki na visu,bangili huku wengine wakiviuza kwa wanaoununua chuma chakavu.

Aidha Shirika hilo limeahidi zawadi nono kwa mwananchi atakayetoa taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa waharibifu na wezi wa miundombinu hiyo na kuwafichia siri watoa taarifa.Amesema,serikali imekuwa ikijitihadi sana kuboresha miundombinu yake,hata hivyo baadhi ya watu wachache wanarudisha nyuma juhudi hizo kwa kuharibu kwa makusudi miundombinu ya umeme na kuisababishia Serikali hasara kubwa.

Ameiomba jamii kushirikiana na Shirika la Umeme (TANESCO) kulinda na kuwa walinzi wa miundombinu ya umeme kwani nishati hiyo ina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa.

Afisa Upelelezi kutoka Jeshi la Polisi wilaya ya Babati Said Ramadhani amesema kosa la kuharibu au kuiba miundombinu ya TANESCO ni Uhujumu Uchumi hivyo adhabu yake ni kifungo na usafiri uliotumika katika uhalifu huo hutaifishwa kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1984 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002 na 2019.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents