HabariSiasa

Deni la serikali hadi Aprili 2022 ni trilioni 69.44

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba leo amewasilisha bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha wa 2022/2023.
Dkt. Mwigulu Nchemba amesema hadi Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 69.44 ikilinganishwa na shilingi trilioni 60.72 kipindi kama hicho mwaka 2021.
“Hadi Aprili 2022, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 69.44 ikilinganishwa na shilingi trilioni 60.72 kipindi kama hicho mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 14.4. Kati ya kiasi hicho, deni la nje lilikuwa shilingi trilioni 47.07 na deni la ndani lilikuwa shilingi trilioni 22.37. Ongezeko la deni la Serikali lilitokana na kupokelewa kwa mikopo mipya kutoka vyanzo vyenye masharti nafuu na ya kibiashara kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.” Dkt. Mwigulu Nchemba.
Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, serikali inatarajia kutumia shilingi trilioni 41 sawa na ongezeko la asilimia 8.1 ya bajeti inayomalizika ya mwaka wa fedha wa 2021/2022.Bajeti ya serikali iliyoidhinishwa na bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022 ilikuwa shilingi trilioni 37.9 ambapo kati ya fedha hizo shilingi trilioni 23 zilitengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 14.9 zilikuwa ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.

Katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha baadhi ya mambo yaliyozingatiwa ni ongezeko la mishahara, ajira mpya, upandishaji wa madaraja kwa watumishi wa umma na sensa ya watu na makazi inayotarajiwa kufanyika mwezi Agosti 23 mwaka huu.

Related Articles

Back to top button