Tragedy

Details: Aliyetobolewa macho Buguruni Sheli aeleza yaliyomsibu siku hiyo

Kuna msemo unaosema hakuna aijuae kesho zaidi ya Mungu pekee, na pia kuna wakati mwingine wahenga husema kesho haina rafiki. Hii imetokea kwa Said Ally kijana ambaye hakuijua kesho yake iko vipi na hakuwahi kufikiria ipo siku atapoteza macho yake katika tukio lililomtokea Buguruni Sheli jijini Dar es Salaam na kuchomwa visu baadhi ya sehemu za mwili wake.

14533643_1696597050660248_6514314186472816640_n

Jumapili, amesimulia mbele ya mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipoenda katika eneo lake analoishi kumueleza yaliyomkuta mpaka kupoteza uwezo wake wa kuona tena.

“Mheshimiwa nimeumia sana tena sana,” alisema. “Ni kitu ambacho mimi mwenyewe sijawahi kukitegemea katika maisha yangu, katika maisha yangu najua ipo siku ntakufa, lakini si kuchomwa visu vile mbele ya watu zaidi ya 40. Nilikuwa natoka ofisini Tabata huwa nafunga ofisi saa nne saa nne na nusu kulingana na jinsi wateja wangu wanavyokuwa, nilifunga saa nne siku hiyo nikaa barabarani nikasubiri usafiri, nikaona magari yanachelewa nikawa nataka niwahi nyumbani nikameze dawa ya matonsensi nikaona magari yanachelewa nikaona nipande Bajaj. Mwenye Bajaj akasema anaenda Buguruni, basi mi nikasema utaniacha relini kwasababu najua ni karibu na njia ya kuja huku. Kufika mazingira ambayo yanaitwa Tabata Barakuda, akasema aah kwasababu abiria uko mmoja acha nikushushe hapa Buguruni Sheli, upate magari ya kwenda Ubungo,nikakubali akasema kwasababu magari yanayoenda Tabata reli yapo mengi,” alisimulia Said.

“Wakati tumeenda Buguruni Sheli tunatoka na njia hii hapa ya kwa Mnyamani akanishusha, nikamlipa hela yake ili nichukue magari ya kwenda Ubungo, wakati napandisha naangalia kulia kwangu ni mapema mno ilikuwa saa nne inaenda na dakika kama 30 hivi ni mapema mno, nikaona kuna wauza kuku, nikasema ngoja ninunue kuku watasaidia siku yoyote nyumbani wakihitaji chakula wawe wanakula, tena wapo wafanyabiashara wengi kila mtu ananiita njoo hapa njoo hapa, nikaangalia mahali pana kuku nzuri nikasimama wakati natoa pesa nimpe muuza kuku, mkono wa kushoto nikatoa elfu 32 nikampa muuza kuku elfu 11, nikabakisha elfu 21, huku pesa iliyokuwa kwenye waleti sikuigusa. Nilikuwa nimesimama muda huo akatokea mtu akasimama kwenye bega la kulia ananiambia ‘bro mimi nina shida’ nikamwambia ‘bro ongea shida yako kabla sijatoka hapa maana nikitoka hapa sina mtu wa kumsikiliza kwasababu Buguruni sina ninayemjua halafu huwa sina kawaida ya kuja Buguruni.’ Basi hajajibu kitu,nikawaangalia wale wauza kuku nikidhani labda kuna ishara watanipa kuhusu yule mtu hakuna ishara yoyote walioitoa wakawa wanaendelea na kazi zao kama kawaida, basi nikajua tu yule mtu huenda ataomba hela tu labda hajakula,” aliendelea.

“Nikashtukia napigwa kisu cha bega la kushoto cha haraka haraka nikapigwa mgongoni nikapigwa begani tena,nikapiga kelele ‘jamani nisaidieni mwizi’ kwasababu nikajua atakuwa mwizi, akanipiga kisu cha tumbo anachoma halafu anakata, anachoma halafu anainua kisu, akanipiga visu vya haraka haraka kama 7 hivi, nasema ‘nisaidieni’ yule mwizi ndo anasema ‘hakuna atakayekusaidia.’ Lakini kiukweli hakuna mtu aliyeshika na butwaa pale katika wale wauza kuku na watu wapo zaidi ya 40. Kuna wamama wauza vyakula wapo wengi sana, hakuna aliyeshikwa na butwaa, nikaanguka pale maskini ya Mungu, wakati naaanguka kuna vitu nilikuwa najiuliza nini kwanza kimenileta huku na nani atatoa taarifa nyumbani kwaba mimi nimevamiwa na mwizi nimepigwa visu mbele za watu na hakuna aliyenisaidia? Akatoa hela kwenye wallet na wallet ilikuwa na laki 3 tu, huku mkononi nilivaa cheni akakata zote na nyingine nilivaa mkononi kama unavyoona mkono wote umechubuka, mpaka t-shirt niliyokuwa nimeivaa akaivua, wakati ananivuta t-shirt bado niko mzima naona sema sina uwezo na sina wa kunisaidia, ananivuta mkono wa kushoto ananivutia barabarani pale nikazimia. Sasa kuna watu pale walikuwa wanaona, kuna dogo mmoja yeye tena alikuwa anaendesha pikipiki, akasema ‘we bro wakati wanakufanyia vitu vibaya hakuna mtu aliyekusaidia mimi nilikuwa naona hakuna aliyediriki kukusaidia,” aliendelea kufafanua.

“Yule bwana akanikuvuta barabarani wakati ashachukua kila kitu ili nigongwe na gari, gari ya kwanza ilipita ilikuwa ni ya jamaa yangu mimi ambaye tumepanga yaani yeye ana fremu pale ambapo mimi nina biashara yangu na yeye ana fremu akasema ‘mimi sikujua kama ni wewe’ lakini nilishtukia kuna mtu hapo kagalagala barabarani kabisa akapiga breki akapita. Kuna mama mwingine akaja kabisa akapiga honi yule mtu ambaye ni muuaji anaruhusu ile gari inigonge. Lakini yule mama akanizunguka, watu wanaona kila kitu lakini hakuna mtu wa kunisaidia, yule dogo anasema kuna defender yaani gari ya polisi Buguruni anasema wakaiita wakasema kuna maiti pale imelala wakapita mara ya kwanza, mara ya pili kuna mtu alipita akasema mimi ni raia mwema nimekuja kukusaidia hapo ishafika saa tano, wakati yule kanipeleka barabarani anaona sigongwi na gari wakati akishakupeleka barabarani anataka ugongwe na gari apoteze ushahidi, alivyonivutia barabarani hapo tayari alikuwa kishawatolea ushahidi wauza kuku pale ili siku nyingine mtu yoyote akija asijue, kanileta barabarani na gari akaona zinanipita akanitoboa macho, akawa bado hajaondoka na watu wanamuangalia,” alisema.

“Akaja kwa mara ya pili akaja mtu akaniambia ‘nimekuja kukusaidia haya taja namba zako nikataja namba anawapigia, mimi defender ndo imekuja kunichukua pale yule bwana amesimama pembeni watu wanamuona, ina maana na wale maaskari wanamuona wamenipakia mimi kwenye ile defender wakanipeleka mpaka polisi kutoa maelezo nikawaelezea kama nilivyoeleza hapa wakanipa PF3. Nikapelekwa kwanza Amana baada ya kupelekwa pale wakaja ndugu zangu. Nasikia kwa mbali kama nipo kwenye ambulace, yaani nimeumia, nimeumia sana kupita maelezo. Maana hata tumbo lenyewe nikikuonyesha utasema yaani mdogo wangu umeponajeponaje mpaka sasa hivi naongea! Yaani nimeumia vibaya mheshimiwa, vibaya mno.

Kitu kingine ambacho mimi kinanishangaza yaani mheshimiwa kote huku mgongoni ni visu yaani nimeumia sana , huku begani hapa vyote ni visu, hivyo visu nilipigwa mbele za watu na sio uchochoroni na nilikuwa mteja nilienda kununua vitu pale. Basi akatoka polisi pale Buguruni akaja Muhimbili kumpa maelezo vizuri, akatoka na ndugu zangu akasema ngoja nikawakamate, kufika pale kituoni wenzake wakamrusharusha wakapewa mpelelezi mwingine huyu dada muache,kama huyo ni brothermen atakuwa kafumaniwa, wakati kumbe wao matatizo yote yale wanayajua na pale sio mimi mtu wa kwanza alishaua, basi nimeumia sana bro maana yake niliumia kupita maelezo kwasababu nina familia, nina watoto na nina wazazi ambao walikuwa wananitegemea mpaka sasa nipo hivi sijui nani atanisaidia, na sijui nasaidiwa na nani niweze kuona maana yake vidonda vingine vinaponapona, macho sijui ntasaidiwa wapi, maana yake nikaakaa kule hospitali, nikatoka, nikaenda kwanza CCBRT wakasema wewe haya macho wameshakutoa sijaamini,” aliongeza kwa uchungu.

“Nikaenda KCMC kwenda hapo nikapata muda kidogo wa kuongea na madaktari, amenitoa nyuzi ambazo zilikuwa kwenye macho humu japokuwa kuna moja ameisahau lakini alinipa huduma nzuri sana, na akaniambia ‘sisi bwana ingekuwa ni jicho ambalo wamelipasua kwa muda huo huo sisi tungelishona na kulihudumia lakini lakini kukusafisha washakusafisha na sisi uwezo wa kukuwekea jicho lingine uwezo huo hatuna ila mishipa bado iko salama.’ Lakini uwezo wa kukuwekea jicho lililokuwa hai uwezo huo hatuna, macho tuliyokuwa nayo sisi ni ya bandia ambayo ukitaka kulala usiku unayatoa na mchana hayafanyi kazi, nikamwambia basi sawa,nimerudi hapa lakini kiukweli mheshimiwa nilikuwa naomba nipate msaada hata kama kuna sehemu kuna uwezekano hata wa kutengeneza jicho moja mimi nikaona basi ninaweza nikafanya kazi familia yangu ikaishi vizuri. Lakini kwa sasa hivi naumia sana mheshimiwa, kwasababu kila nikiangalia mi naona ni usiku wa manane,” alieleza.

Kupitia Instagram, Jumatatu Makonda amesema ameongeza na madaktari wa Muhimbili kutafuta namna ya kumsaidia ili aweze kuona tena.

Amesema:

Nimeongea na Madaktari bingwa ktk hospital yetu ya Mhimbili na kesho nampeleka ndg yetu ili jopo la Madaktari wampime na matokeo yatakayopatikana yatatupatia hatua sahihi juu ya macho ya ndg yetu yaliyotobolewa. Natamani ndg yangu Said aone tena.

BY: EMMY MWAIPOPO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents