Dk; Biteko: Upatikanaji wa mafuta nchini unaimarika na biashara hiyo inazidi kuwa ya uwazi

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema kuwa upatikanaji wa mafuta nchini unaendelea kuimarika na kwamba biashara hiyo inazidi kuwa ya uwazi.
Dkt. Biteko ameeleza hayo Aprili 9,2025 jijini Dodoma wakati aliposhiriki katika uzinduzi wa Taarifa za Maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2023/24 iliyoandaliwa na Bodi ya Wakurugenzi na Wafanyakazi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).
Amesema pamoja na hali hiyo bado kuna kazi inapaswa kufanyika ili kuhakikisha bei ya mafuta nchini inakuwa halisi na kusisitiza kuwa wakati serikali inaoata faida kidogo, ni muhimu wananchi wanapotumia bidhaa hiyo ya mafuta wapate kwa bei nafuu kidogo.
“Pamoja na kuimarika kwa biashara ya mafuta nchini ni muhimu watendaji wa sekta ya nishati kuhakikisha mnatekeleza majukumu yenu kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kutoa huduma bora kwa wananchi. hapa nimeona kuna wafanyabiashara wa mafuta huwa kuna muda wananiambia EWURA wanawabana, nadhani moja ya kazi ya EWURA ni kubana kidogo.
“Niwaombe EWURA muendelee kubana katika sekta hii ya mafuta lakini kwa kuzingatia mazingira ya biashara ili kuepuka kutofilisika kwa wafanyabishara katika sekta ya nishati,” amesema Dk. Biteko
Aidha Dk. Biteko amesema Serikali inaendelea kujenga vyanzo vipya vya umeme na kuweka msukumo mkubwa katika uwekezaji wake ili kukabiliana na hatari ya uhaba wa umeme inayoweza kutokea zisipofanyika jitihada za makusudi na za haraka.
“Mahitaji ya umeme yameongezeka hadi megawati 254 ambapo ni sawa na kujenga mradi mwingine kama wa Kidatu, ifikapo mwaka 2030, mahitaji ya juu ya umeme yatakuwa megawati 4,878 na mwaka 2025 mahitaji ya juu ya umeme yatafikia megawati 8,055 taarifa hii inaonesha hatari kama hatutachukua hatua,” amebainisha Dkt. Biteko.

Kwa upande wa sekta ndogo ya gesi asilia, Dkt. Biteko amesema kama zilivyo sekta nyingine za nishati kwa mujibu wa taarifa hiyo imeonesha kuwepo ongezeko la matumizi ya gesi asilia viwandani, majumbani na kwenye vyombo vya usafiri. Aidha, vituo vya kujaza gesi iliyoshindiliwa kwenye magari (CNG) vimeongezeka.
Katika hatua nyingine, Dk. Biteko amesema pamoja na jitihada za Serikali kuhakikisha upatikanaji wa nishati ya uhakika ya umeme, mafuta na gesi asilia bado sekta inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwepo mabadiliko ya tabia nchi na uharibifu wa mazingira, upungufu na uchakavu wa miundombinu.
Ametaja changamoto zingine ni za rasilimali fedha kwa ajili ya uwekezaji na za maendeleo ya sayansi na teknolojia. Hata hivyo, ili kuondokana na changamoto hizo amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, itaendelea kuhakikisha inaboresha, inaimarisha, inarahisisha na inawezesha upatikanaji wa nishati safi kwa Watanzania wote.
“Namshukuru sana na kumpongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa mchango mkubwa katika kuimarisha sekta ya nishati. Chini ya uongozi wake, tumeshuhudia maendeleo makubwa katika sekta hii ikiwemo ukamilishwaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na kielelezo ambayo imeongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika nchini, upatikanaji wa bidhaa za petroli, pamoja na ongezeko kubwa la matumizi ya gesi asilia hususani kwenye magari,” amesisitiza Dkt. Biteko.
Aidha Dk. Biteko ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi na Wafanyakazi EWURA kwa uandaaji wa Taarifa hiyo za Maendeleo ya Sekta ya Nishati kwa Mwaka 2023/24 kwa kuwa zina umuhimu mkubwa kwa Serikali katika kufanya maamuzi, kwani zinasaidia kuona mwenendo wa sekta ya nishati kwa kuonesha hali ya sekta hiyo ya nishati, mafanikio, changamoto na fursa zilizopo katika kuiendeleza.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amesema; “Naendelea kumpongeza Rais Samia kwa kazi kubwa inayofanyika katika sekta ndogo ya nishati na usimamizi mzuri wa Dkt. Biteko unaowezesha kupata mafanikio yote haya,” ameeleza Kapinga.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi EWURA, Profesa Mark Mwandosya, ameishukuru na kuipongeza Serikali kwa uwekezaji mkubwa inaoendelea kuufanya katika sekta ya nishati.
“Hii miradi mikubwa hasa ya umeme mfano Bwala la Julius Nyerere inachukua muda mrefu hadi kukamilika kwake hivyo ni kiashiria kwamba tuanze sasa kutekeleza miradi mingine ili baada ya miaka kadhaa tusijekupata changamoto ya umeme,” amesema Profesa Mwandosya.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji ( EWURA), Dkt. James Andilile amesema kuwa uzinduzi wa taarifa hizo ni takwa la kisheria na tayari wameshafanya hivyo kwa upande wa sekta ya maji.
Amesema katika sekta ndogo ya umeme hadi kufikia Juni 2023/2024 uzalishaji wa umeme ulikuwa megawati 2,411 na sasa umefikia megawati 4,032.“Kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme huduma imeimarika na sasa changamoto iliyokuwepo imeondolewa.
“Kuhusu gharama za bei ya umeme kutokana na uwekezaji katika miundombinu hali ya fedha TANESCO imeendelea kuimarika na mwaka wa tatu mfululizo imetengeneza faida kutokana na usimamizi wa Serikali wa kuondokana na mitambo ya kukodi ya kuzalisha umeme,” amesema Dkt. Andilile
Ameongeza kuwa katika sekta ya mafuta hadi kuishia Juni 2023/2024 vituo vya mafuta vilikuwa 2,361 sawa na ongezeko la asilimia 10, kukiwa na vituo 480 vijijini sawa na ongezeko la asilimia 12. Pia, kuhusu gesi asilia amesema katika mwaka 2020/2023 vyombo vya moto vilivyokuwa vinatumia gesi asilia vilikuwa 7,000 na kufikia Machi mwaka huu vimefikia 15,000 ikiwa ni sawa na asilimia 49.
Written by Janeth Jovin




