HabariSiasa

Dkt Slaa Mahakamani tena leo

Mwanaharakati Dkt. Willbroad Slaa yuko Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam leo, Ijumaa Januari 24.2025 kwa ajili ya kufuatilia shauri lake alilofungua Mahakamani hapo akiiomba Mahakama hiyo kufuta shauri la msingi lililofunguliwa na Jamhuri/ serikali dhidi yake kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Hata hivyo licha ya kwamba shauri hilo lilitarajiwa kuanza kusikilizwa leo Mahakamani hapo kuanzia saa 03 asubuhi lakini baada ya Jaji kuingia kwenye chumba cha Mahakama huku pande zote (upande wa waleta maombi na wajibu maombi) wakiwa tayari kuanza kusikiliza, ghafla Mawakili wa upande wa utetezi (Mawakili wa Serikali) wakaileta hoja ya kuoomba Mahakama kuliondoa shauri hilo Mahakamani hapo kwa kuwa halijakidhi vigezo kadhaa vya kisheria vya kuweza kusikilizwa

Hoja hiyo imeibua sintofahamu na kuanzisha mivutano mipya ya kisheria baina ya Mawakili wa pande zote mbili, ndipo baadaye Jaji anayesikiliza shauri hilo aliamua kuhairisha kesi hiyo hadi saa 05:30 asubuhi ya leo huku akitumia nafasi hiyo kuwataka upande wa waleta maombi (upande wa Dkt. Slaa) watakaporejea wawasilishe ushahidi/ hoja za kisheria zitakazojibu mapingamizi yaliyoletwa na upande wa utetezi (Mawakili wa Serikali)

Ikumbukwe kuwa Dkt. Slaa ambaye pia ni Mwambata wa ‘Sauti ya Watanzania’ alifikishwa kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jioni ya Ijumaa ya Januari 10.2025, hiyo ikiwa ni baada ya kukamatwa na maafisa wa Jeshi la Polisi usiku wa Januari 09.2025 nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam

Baada ya kufikishwa Mahakamani hapo Dkt. Slaa anayekabiliwa na shtaka moja la kusambaza taarifa za uongo katika mtandao wa kijamii wa X zamani ukijulikama kama Twitter, ambapo alisomewa kesi hiyo ya jinai namba 993 ya mwaka 2025 na jopo la Mawakili watatu (3) wa serikali wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Clemence Kato akishirikiana na Tumani Mafuru na Abdul Bundala, ambao kwa pamoja waliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa mtuhumiwa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao namba 14 ya mwaka 2015

Siku chache zilizopita, katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ndogo ya Dar es Salaam Dkt. Slaa ambaye pia amewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden alifungua shauri lingine akipinga ‘danadana’ za kutopatiwa dhamana anazofanyiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu chini ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki anayesikiliza shauri lake, hivyo kuiomba Mahakama Kuu kuingilia kati na kumpatia dhamana, shauri ambalo maamuzi yake yanatarajiwa kutolewa Jumatatu ya juma lijalo na Jaji Anold Kirekiano, hii ya Leo ni nyingine mpya aliyofungua Mahakama Kuu akiiomba kufuta kabisa shauri hilo lililofunguliwa na Jamhuri dhidi yake kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu

Katika mashauri hayo yote, Dkt. Slaa anawakiliahwa na jopo la Mawakili wakiongozwa na Peter Madeleka, Hekima Mwasipu, Edson Kilatu, Mwanaisha Mndeme, Paul Kisabo na wengineo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents