DRC yawatuhumu waasi wa M23 kukiuka makubaliano
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limewashutumu waasi wa M23 kwa kuwaua raia 50 na kukiuka makubaliano ya siku tano ya kusitisha mapigano mashariki mwa nchi hiyo.
Jenerali Sylvain Ekenge amesema kundi la M23 limekuwa likifanya mauaji ya kikatili, na kwamba siku ya jumanne walivamia kijiji cha Kishishe kilichoko kilomita 70 kaskazini mwa mji wa mashariki wa Goma na kuwauwa raia 50 wa Kongo.
Kundi la M23 lilijibu kwa taarifa iliyoeleza shutuma za mauaji ya Kishishe kama “madai yasiyo na msingi” na kusisitiza kuwa hawajawahi kuwalenga raia.
Usitishwaji wa mapigano ulianza katika jimbo la Kivu Kaskazini mwishoni mwa juma kufuatia mkutano kati ya DRC na jirani yake Rwanda. Lakini vyanzo vya habari vimesema kwamba mapigano yalianza tena jana Alhamisi huko Kirima takriban kilomita 10 kutoka mji wa Kibirizi.