
Katika mradi wa utafiti wa Jeshi la Wanamaji la Uingereza (Royal Navy), wahandisi huko Somerset wanaunda helikopta ambayo itakuwa inajirusha yenyewe – bila hitaji la wanadamu kuiendesha hata kwa mbali.
Zipo helikopta zisizo na marubani, lakini zote huendeshwa na marubani wakiwa mbali katika vyumba vya udhibiti kwenye meli au kambi ya jeshi.
Helikopta ya majaribio ya Proteus inaundwa na timu ya kampuni ya Leonardo Helicopters UK, huko Yeovil, ambayo itaruka yenyewe na kutekeleza misheni yenyewe. Inaaminika kuwa ni ya kwanza ya aina hii duniani.
“Ni kwa lengo la kutowaweka watu katika hatari,” anasema Nigel Colman, mkurugenzi mkuu wa Leonardo Helicopters UK, watengenezaji wakuu wa helikopta nchini Uingereza.
Bw Colman anazijua helikopta. Alikuwa rubani wa Jeshi la Anga la Uingereza (RAF), kwa miaka 30, hadi kufikia kuwa na nyota mbili, na kusimamia Kamandi ya Pamoja ya Vyombo vya Angani vya Jeshi la Ardhini, Majini na Angani vya Uingereza.
Wengi hufikiria helikopta katika misheni za mapigano, ni kurusha mabomu au kusafirisha vikosi maalumu karibu na safu za adui. Lakini helikopta nyingi hufanya kazi za kawaida, kama kuhamisha mizigo kutoka katika meli moja hadi nyingine, au kutoka katika meli hadi ufukweni.
“Watu kama mimi tumetumia miongo kadhaa kufanya safari za hatari,” anasema Colman.
“Ikiwa si lazima kuhatarisha maisha, tunaweza kuirusha hii kwa saa nane, haihitaji binadamu kuindesha. Hakuna mambo mengi ya kushughulika nayo.”
Itafanya misheni gani?

Kazi ya kawaida itakuwa ni kudondosha maboya ya sonar baharini, ambayo hutumiwa kusikiliza sauti za nyambizi. Marubani hufanya kazi hii mara kwa mara, na kila safari ina hatari.
Helikopta hiyo ya Proteus itapaa kutoka kwenye manowari ya Jeshi la Wanamaji, kwa kutumia kodi zilizosetiwa, kwa ajili ya kudondosha maboya, kisha kurudi kwenye monowari. Yote hayo, bila binadamu kuindesha helikopta hiyo.
Colman anasema: “Itajiendesha yenyewe. Hakuna mtu atakayesimama pembeni na rimoti shingoni, akibofya vitufe.”
Na ikiwa hali ya misheni itabadilika, yaani dhoruba ikatokea, au chombo kisicho tarajiwa kitaonekana. Anajibu kwa kusema:
“Itakuwa na taarifa zote inazohitaji ili kuchukua mwelekeo mpya. Ili kuzuia vitisho, kuzuia migongano, na chochote kinachohitajika.”
Wahandisi wa programu za kompyuta wanazalisha mfumo wa namna helikopta hiyo itakavyo fanya kazi. Katika mfano mmoja, helikopta inaoneka ikitaka kudondosha boya, lakini kuna boti ndogo ya wavuvi. Kamera ya chini ya helikopta inachukua picha, na kubadilisha mwelekeo na sehemu ya kudondosha boya.
Helikopta hii inatengenezwa huko Yeovil kwenye kiwanda ambacho kimeunda helikopta kwa miaka 80. Kwa sasa kampuni hiyo inamilikiwa na Leonardo. Kwa jumla, zaidi ya 50% ya helikopta zinazoendeshwa na vikosi vya jeshi la Uingereza zimeundwa katika kiwanda hiki.

Watu wanaofanya kazi kwenye mradi huu mpya wanajivunia mradi huo. Kando na vifaa vya elektroniki vya hali ya juu na kazi za kidigitali, pia kuna bisibisi na spana nyingi.
Victoria Thorpe alipata nafasi ya kujiunga na mradi huo, katika kitengo cha ununuzi wa vifaa. Anasema: “Inafurahisha kufanya kazi kwenye kitu kipya, na tunashirikiana na kampuni nyingi za ndani ambazo zinatupatia vifaa.”
Proteus ni programu ya utafiti ya Jeshi la Wanamaji. Helikopta ya aina hii hazitazalishwa kwa wingi, lakini wataalamu wanasema nchi zote zinabuni vyombo vya angani ambavyo vinajiendesha vyenyewe.
David Gailbraith, Prof wa Vita na Teknolojia katika Chuo Kikuu cha Bath, anasema: “Majeshi yanazidi kutegemea mitambo inayojiendesha yenyewe (automatiki), ili kufanya kazi ambazo ni hatari sana, kwahiyo ni jaribio la kuondoa hatari kwa binadamu.
Timu hiyo inatarajia helikopta mpya itapaa “katika majira ya joto.” Mahali itakapopaa itakuwa ni siri, mbali na miji au vijiji. Na wana imani itafanikiwa.
“Tutaiunda, itafanya kazi yake na itakamilisha misheni yake,” anasema Colman.
cc:BBC Swahili