Habari

Dawasa yakutana na wananchi wa Golani kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) imekutana na kuzungumza na wananchi wa Mtaa wa Golani, Kata ya Kimara, Wilaya ya Ubungo kwa lengo la kutatua changamoto ya upatikanaji huduma ya maji mtaani hapo.

Akizungumza kwa niaba ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Dawasa, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano, Everlasting Lyaro amewatoa hofu wananchi wa Golani nikiwaambia Mamlaka inatambua changamoto ya maji katika mtaa huo na zipo hatua za muda mfupi na mrefu ambazo zitachukuliwa kuhakikisha kila mwananchi anapatiwa huduma ya majisafi.

“Kwanza tuwaombe radhi wananchi wa hapa Golani kwa changamoto ya maji mnayoipitia, tunatambua maji ni haki ya kila mmoja wetu kupata, Mamlaka inatambua changamoto hii na hapa leo tumekuja kuwaeleza hatua tatu tutakazochukua kutatua changamoto ya maji hapa Golani,” amesema Lyaro na kuongeza

“Pia kwa kuanza Mamlaka italeta matenki 5 yenye ujazo wa Lita 10,000 kila moja na kuyajaza maji yatakayouzwa kwa bei elekezi zoezi litakalofanyika mapema Januari 15, 2025 ili kukabiliana na changamoto hiyo, lakini pia tutaratibu mgao wa maji katika eneo hili ambapo watapata maji mara tatu kwa wiki, Alhamisi, Jumapili na Jumatatu,” amesema

Aidha Lyaro amesema changamoto hiyo ya maji itatatuliwa kwa mpango wa muda mrefu wa kujenga kituo cha kusukuma maji eneo la kwa mama Stela na kusaidia maji kufika sehemu mbalimbali zilizokua hazipati huduma awali.

Kwa upande wake, Meneja wa Mkoa wa kihuduma DAWASA Kinyerezi amesema watumishi hawatakaa ofisi bali watatoka kuwafikia wananchi na kuhakikisha yaliyopangwa katika kikao hicho yanatekelezwa.

Rajabu Said, Mkazi wa Golani ameshukuru jitihada zinazofanyika kuhakikisha changamoto ya maji mtaani hapo inakwisha na sasa wanaanza kupata matumaini tena ya huduma ya maji na kuondokana na ununuzi wa maji kwa watoa huduma binafsi unaowagharimu fedha nyingi.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents