HabariTechnology

Elon Musk kuachia ngazi nafasi ya mtendaji mkuu Twitter

Elon Musk amesema atajiuzulu kama afisa mkuu mtendaji wa Twitter atakapompata mtu “mjinga kiasi cha kuchukua kazi hiyo”.

Bilionea huyo aliahidi mapema kutii matokeo ya kura ya maoni ya Twitter ambayo 57.5% ya watumiaji walipiga kura ya “ndio” kumtaka kuacha jukumu hilo.

Anasema bado ataendesha timu za programu na seva baada ya mbadala wake kupatikana.

Mabadiliko kwenye jukwaa hilo tangu Musk kushika usukani yamekosolewa sana.

Tangu Bw Musk aliponunua mtandao huo wa kijamii mwezi Oktoba, amewafuta kazi takriban nusu ya wafanyakazi wake na kujaribu kusambaza kipengele cha kulipia cha uthibitishaji cha Twitter kabla ya kusimamisha mpango huo. Kipengele hicho kilizinduliwa tena wiki iliyopita.

Mashirika ya kupigania uhuru wa kiraia pia yamekosoa mbinu yake ya kudhibiti maudhui, yakimtuhumu kuchukua hatua ambazo zitaongeza matamshi ya chuki na habari potofu.

Siku ya Ijumaa, Bw Musk alilaaniwa na Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya kutokana na uamuzi wa Twitter wa kufuta akaunti za baadhi ya wanahabari wanaoripoti kuhusu kampuni hiyo ya mitandao ya kijamii.

Umoja wa Mataifa uliandika kwenye Twitter kwamba uhuru wa vyombo vya habari “sio mchezo”, wakati EU ilitishia Twitter kwa vikwazo.

Hii ni mara ya kwanza kwa bilionea huyo kujibu kura ya maoni iliyoanzishwa Jumapili akiuliza ikiwa anafaa kujiuzulu. Kupata mtu wa kuchukua nafasi hiyo kunaweza kuwa changamoto, kulingana na Bw Musk.

“Hakuna anayetaka kazi hiyo ambaye anaweza kuweka Twitter hai,” aliandika kufuatia kura hiyo.

Related Articles

Back to top button