Ushahidi wa unyanyasaji ulionea na mateso kutoka kwa mwanzilishi wa mojawapo ya makanisa makubwa ya kiinjili ya Kikristo duniani umefichuliwa na BBC.
Makumi ya waumini wa zamani wa Kanisa la Synagogue Church of all Nations – watano Waingereza – wanadai ukatili, ikiwa ni pamoja na ubakaji na utoaji mimba kwa lazima, uliofanywa na marehemu TB Joshua wa Nigeria.
Madai ya unyanyasaji katika eneo la siri la Lagos yamedumu kwa takriban miaka 20.
Kanisa la Synagogue Church of All Nations halikujibu madai hayo lakini lilisema madai ya hapo awali hayana msingi.
TB Joshua, aliyefariki mwaka wa 2021, alikuwa mhubiri na mwinjilisti mwenye mvuto mkubwa na mwenye mafanikio makubwa ambaye alikuwa na wafuasi wengi duniani.
Matokeo ya BBC katika uchunguzi wa miaka miwili ni pamoja na:
- Masimulizi mengi ya watu waliojionea matukio ya ukatili wa kimwili au mateso yaliyofanywa na Joshua, ikiwa ni pamoja na matukio ya unyanyasaji wa watoto na watu kuchapwa viboko na kufungwa minyororo.
- Wanawake wengi wanaosema walinajisiwa na Joshua, huku baadhi wakidai kuwa walibakwa mara kwa mara kwa miaka mingi ndani ya boma hilo.
- Tuhuma nyingi za kutoa mimba kwa lazima ndani ya kanisa kufuatia tuhuma za ubakaji na Joshua, akiwemo mwanamke mmoja ambaye anasema alitolewa mimba mara tano.
- Simulizi nyingi za moja kwa moja zinazoelezea jinsi Joshua alivyodanganya kuhusu “uponyaji wake wa miujiza”, ambao ulitangazwa kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote.
Mmoja wa waathiriwa, mwanamke wa Uingereza, anayeitwa Rae, alikuwa na umri wa miaka 21 alipoacha shahada yake katika Chuo Kikuu cha Brighton mnamo 2002 na kuandikishwa katika kanisa. Alitumia miaka 12 iliyofuata kama mmoja wa wale wanaoitwa “wanafunzi” wa Yoshua ndani ya boma lake la kifahari huko Lagos.
“Sote tulidhani tuko mbinguni, lakini tulikuwa katika hali inayofanana na ya kuzimu, na huko kunatokea mambo mabaya,” aliiambia BBC.
Rae anasema alinajisiwa na Joshua na kuwekewa aina ya kifungo cha upweke kwa miaka miwili. Dhuluma hiyo ilikuwa kali sana, anasema alijaribu kujiua mara nyingi ndani ya boma hilo.
Kanisa la Synagogue Church of All Nations [Scoan] lina wafuasi wa kimataifa, wanaoendesha chaneli ya TV ya Kikristo iitwayo Emmanuel TV na mitandao ya kijamii yenye mamilioni ya watazamaji. Katika miaka yote ya 1990 na mwanzoni mwa miaka ya 2000, makumi ya maelfu ya mahujaji kutoka Ulaya, Amerika, Kusini Mashariki mwa Asia na Afrika walisafiri hadi kanisani humo nchini Nigeria kumshuhudia Joshua akifanya “miujiza ya uponyaji”. Takriban wageni 150 waliishi naye kama wanafunzi ndani ya boma lake huko Lagos, wakati mwingine kwa miongo kadhaa.