Fundi huyu kutua Simba
Wakati Kikosi cha Simba kikiendelea kufanya vizuri katika ligi kuu Tanzania Bara, Viongozi wa timu hiyo bado hawajaridhika wakitarajiwa kumfuata kiungo mshambuliaji Foday Trawally raia wa Gambia anayekipiga katika klabu ya Centinkaya TSK ya Uturuki.
Habari zilizopatikana juzi Jumapili kutoka ndani ya Klabu ya Simba zimebainisha kuwa mazungumzo baina ya pande mbili yameshaanza na Simba inataka kumpa mkataba wa miaka mitatu mchezaji huyo mwenye miaka 23 ambaye pia ameshazichezea klabu mbalimbali nchini Uturuki ikiwamo Tuzlaspor.
Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimesema kuwa Simba imeamua kuongeza kiungo mshambuliaji anayecheza klabu hiyo iliyoko Ligi daraja la pili nchini humo ili kuwasaidia wachezaji wawili kwenye eneo hilo ambao ni Jean Charles Ahoua na Awesu Awesu.
Dirisha dogo la Usajili litafunguliwa mwezi Disemba 15 na Simba itaanza rasmi kuwatangaza wachezaji ambao watatua kuongeza nguvu kikosini.