Habari

Gari la zimamoto na uokoaji lawasili Gairo kuimarisha huduma za dharura

Gari jipya la zimamoto na uokoaji limewasili wilayani Gairo kufuatia maombi ya wakazi wa eneo hilo yaliyowasilishwa kupitia Mbunge wao, Ahmed Mabukhut Shabiby, kwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha huduma za dharura wilayani humo na kuongeza usalama wa wananchi dhidi ya majanga mbalimbali yanayoweza kujitokeza katika maeneo ya makazi, biashara na taasisi za umma.

Akikabidhi gari hilo kwa watendaji wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mara baada ya kuwasili wilayani humo, Mbunge wa Gairo, Ahmed Mabukhut Shabiby, amesema ujio wa gari hilo ni hatua muhimu katika kuboresha miundombinu ya huduma za uokoaji.

Amesema gari hilo litasaidia kuzuia na kupambana na majanga ya moto pamoja na dharura nyinginezo, ikiwemo ajali na matukio yanayohitaji uokoaji wa haraka kwa wananchi.

Aidha, ameishukuru serikali kwa kuitikia ombi la wananchi wa Gairo na kusisitiza kuwa upatikanaji wa gari hilo ni matokeo ya ushirikiano kati ya viongozi na wananchi katika kutatua changamoto za maendeleo.

Kwa upande wake, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wilaya, Zengwe A. Zengwe, amesema kabla ya kupatikana kwa gari hilo kulikuwa na changamoto za kufika kwa wakati katika matukio ya dharura.

Amebainisha kuwa kumekuwa na matukio ya watu kutumbukia kwenye mashimo ya vyoo hasa nyakati za mvua, hivyo gari hilo litakuwa mwarobaini wa changamoto hiyo pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli nyingine za uokoaji.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Kaphari Kubecha, amesema utashi mwema wa viongozi wakuu wa serikali umewezesha upatikanaji wa gari hilo, na ameahidi kuwa litatunzwa na kutumika ipasavyo ili liweze kuleta tija iliyokusudiwa kwa wananchi.

Written by Ignas Kabirigi

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents