Hitilafu ya umeme yasababisha treni ya SGR kusimama kwa saa mbili

Shirika la Reli la Tanzania (TRC) limeomba radhi kufuatia hitilafu ya umemem iliyojitokeza kati ya Stesheni ya Kilosa na Kidete na kusababisha treni ya reli ya kiwango cha kimataifa (SGR) iliyokuwa inasafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Dodoma kusimama kwa juda wa saa mbili usiku wa jana Julai 30, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Julai 31,2024 na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano TRC, Jamila Mbarouck amesema taarifa za awali zinaonesha kuwa hitilafu za aina hiyo husababishwa na wanyama (ngedere) au ndege (bundi) wanapogusa nyaya za umeme zilizotandazwa juu ya reli (overhead catenary system).
Imesema hitilafu ilisababisha umeme katika kituo cha kupoozea umeme namba 7 (Godegode) ambao kitaalamu hujulikana kama (Instanteneous Overcurrent Protection Trip) majira ya Saa 4:20 usiku.
“Mafundi wa TRC walifanikiwa kutatua changamoto na kurejesha umeme saa 6:30 usiku na treni kuendelea na safari kuelekea Dodoma na kuwasili Dodoma majira ya saa 7:57 usiku, Shirika la Reli Tanzania linaomba radhi kwa usumbufu,” imesema taarifa hiyo
Written by Janeth Jovin