Aina mpya ya homa ya nyani imesababisha mamia ya vifo katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), na imeenea katika maeneo ya Afrika ya Kati na Mashariki.
Mapema mwezi huu, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza mlipuko huo kuwa dharura ya kiafya kwa umma kimataifa.
Husababishwa na aina mpya na kali zaidi ya mpox inayojulikana kama Clade 1b.
WHO imesema kuhakikisha chanjo zinafika maeneo yenye uhitaji mkubwa, ni jambo muhimu katika kukabiliana na mlipuko huo.
Je, kuna chanjo ya mpox?
Kuna chanjo mbili zinazopendekezwa na WHO za mpox – kwa ugonjwa ambao zamani ulijulikana kama monkeypox. Lakini nchi nyingi bado hazijaidhinisha matumizi ya chanjo hiyo.
WHO inapendekeza chanjo ya MVA-BN na LC16, au chanjo ya ACAM2000 ikiwa hizo mbili hazipo.
Mapema mwezi huu, shirika hilo lilianzisha mchakato wa kuorodhesha chanjo za dharura za mpox ili kusaidia haraka nchi za kipato cha chini.
Uorodheshaji huu unamaanisha mashirika kama vile Unicef na Gavi wanaweza kukusanya na kusambaza chanjo hizo.
WHO kwa sasa haipendekezi chanjo kwa watu wengi. Inapendekeza kuchanja watu walio katika hatari, watu ambao wamekuwa katika mawasiliano ya karibu na mtu ambaye ana mpox na wale katika jamii zilizo na milipuko.
Ikiwa mtoa huduma wako wa afya ataona uko hatarini kwa sababu ya mipango ijayo ya safari, WHO inasema unaweza kuchoma chanjo.
Wiki iliyopita, Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa (ECDC), kilipendekeza wasafiri kupata chanjo ikiwa wanapanga kutembelea maeneo yaliyoathirika barani Afrika.
Wale ambao wamechanjwa dhidi ya mpox hapo awali wanaweza kuchomwa dozi moja tu ya nyongeza, badala ya dozi mbili.
Dozi za chanjo ya nyongeza kwa kawaida hupendekezwa kila baada ya miaka miwili hadi 10, ikiwa mtu ataendelea kuwa katika hatari ya kuambukizwa.
Je, chanjo ya zamani ya ndui inalinda?
Mpox husababishwa na virusi vya familia moja na ndui. Chanjo ya ndui iliyochomwa kwa watu wengi wazee inaweza kutoa ulinzi fulani.
WHO ilitangaza ugonjwa wa ndui kuwa umetokomezwa mwaka 1980 (ugonjwa pekee wa kuambukiza kuwahi kupewa tangazo hilo), na chanjo zikaachwa kutumiwa miongo minne iliyopita.
Kuna chanjo za kutosha za mpox?
Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa kimesema kina mpango wa kupata dozi milioni 10 za chanjo kwa bara hilo kufikia 2025.
DRC na Nigeria zitaanza kutoa chanjo kuanzia wiki ijayo, huku DRC ikitumia dozi kutoka Marekani na Japan, na Nigeria ikitumia chanjo kutoka Marekani.
Waziri wa afya wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Roger Kamba, alisema watoto watapewa chanjo kwanza kwani kiwango cha maambukizi ya mpox, ni kikubwa kwa wale walio chini ya miaka 15.
Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa, kimesema kimefikia makubaliano na kampuni ya kutengeneza madawa kutoka Denmark iitwayo Bavarian Nordic, kutumia teknolojia yake na kuzalisha chanjo katika bara la Afrika.
Hivi karibuni WHO iliwataka watengenezaji wa dawa kutengeneza chanjo za mpox kwa matumizi ya dharura, hata kama chanjo hizo hazijaidhinishwa rasmi.
Nigeria imesema inatarajia kupokea kundi lake la kwanza la chanjo 10,000 kutoka serikali ya Marekani siku ya Jumanne.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo inasema Marekani imeahidi dozi 50,000, huku Japan ikisema itatoa chanjo milioni 3.5.
Je, chanjo ya mpox inafanya kazi?
WHO inasema chanjo ya mpox “hutoa kiwango cha ulinzi dhidi ya maambukizi na ugonjwa mkali.”
Mapema wiki hii, mkurugenzi wa kanda wa WHO barani Ulaya, Dk Hans Kluge, alisema mpox “sio Covid mpya” – kwani inaweza kudhibitiwa kupitia hatua zisizo za kibaguzi kwa umma, na kutoa chanjo kwa wote.
WHO inashauri kuchukua tahadhari ili kuepuka kupata au kueneza mpox baada ya kuchanjwa, kwani inachukua wiki kadhaa kupata kinga baada ya kuchomwa.
Ikiwa utapata mpox hata baada ya kuchanjwa, bado itatoa kinga dhidi ya ugonjwa huo kuwa mbaya na kulazwa hospitalini.