Idadi ya vifo kutokana na kimbunga nchini Ufilipino vyafikia 388

Serikali ya Ufilipino imesema idadi ya waliofariki kutokana na kimbunga kikali kilichoikumba nchi hiyo imeongezeka na kufikia watu 388 leo huku baadhi ya maeneo yalioathirika yakikabiliwa na tishio la kuzuka kwa magonjwa.

Wakati serikali ikishughulika kupeleka chakula, maji na nguo katika maeneo yalioathirika, kitisho kipya kimejitokeza katika siku za hivi karibuni huku watu 140 wakiugua kutokana na kutumia maji machafu.
Waziri wa afya Maria Rosario Vergeire amesema kuwa watu 80 waliugua ugonjwa wa tumbo katika mkoa wa kusini wa Visiwa vya Dinagat, huku watu 54 wakipatiwa matibabu ya kuharisha hospitalini katika kisiwa jirani cha kitalii cha Siargao Vergeire amesema kimbunga hicho pia kimeharibu zaidi ya dozi elfu 4 za kinga ya virusi vya corona na kuvunja hospitali 141 na kliniki ambapo ni 30 tu zilioanza kutoa huduma kamili.


