
Taarifa iliyotolewa na Mchunguzi wa afya wa Kaunti ya LA inaeleza kuwa idadi ya waliofariki hadi kufikia Jumapili ni ishirini na nne (24). Awali, maafisa walisema takribani wengine kumi na sita (16) hawajulikani walipo.
Kumi na sita (16) kati ya waliofariki walipatikana katika eneo la moto la Eaton, huku wanane wakipatikana katika eneo la Palisades.
Moto unaendelea kuwaka katika maeneo matatu karibu na Los Angeles.
Watabiri wa hali ya hewa huko California wanaonya upepo mkali ambao ulisababisha moto karibu na Los Angeles kuwa unatarajiwa kushika kasi tena wiki hii, huku vikosi vya zima moto vikiendelea kujitahidi kudhibiti mioto mitatu ya nyikani.
Maafisa wameonya kwamba baada ya wikendi ya upepo uliopungua kasi kiasi, upepo uliokauka wa Santa Ana utavuma tena kuanzia Jumapili usiku hadi Jumatano, na kufikia kasi ya hadi 60mph (96km/h).
Kabla ya kurejea tena kwa upepo huo, kuna hatua ambazo zimefikiwa kuzuia kuenea kwa mioto mikali ya Palisades na Eaton, ambayo inawaka pande tofauti za jiji.
Wazima moto wa eneo hilo wanasaidiwa na wafanyakazi kutoka majimbo mengine manane, pamoja na Canada na Mexico ambao wanaendelea kuwasili.
Moto mkubwa zaidi ni Palisades, ambao sasa umeteketeza zaidi ya ekari 23,000 na kudhibitiwa kwa 11%.
Moto wa Eaton ni wa pili kwa ukubwa na umeteketeza zaidi ya ekari 14,000. Umedhibitiwa kwa asilimia 27.
Moto wa Hurst umeenea hadi ekari 799 na karibu unadhibitiwa wote kabisa.
Siku ya Jumapili, wazima moto waliweza kuzuia haraka kuenea kwa moto uliokuwa unaanza kuwaka katika Msitu wa Kitaifa wa Angeles, unaozunguka eneo ambalo ni kitovu cha mpango wa anga za juu wa Marekani na una teknolojia ya siri ya juu.