IGP Sirro afanya mabadiliko ya makamanda, Muliro kuwa Kamanda wa Kanda Maalum Dar

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amefanya mabadiliko madogo kwa baadhi ya makamanda wa polisi wa mikoa na makao makuu ya polisi ili kuleta  ufanisi wa utendaji kazi wa jeshi hilo

Katika mabadiliko hayo amemrudisha Dar es Salaam, Jumanne Muliro  kuwa Kamanda wa Polisi wa Kanda ya Maalum Dar es Salaam. Kamanda Muliro anatoka Mwanza na kurejeshwa Dar es Salaam ambako aliwahi kuwa kamanda wa polisi mkoa wa Kinondoni.

Kamanda Muliro amerudishwa Dar es Salaam, kuchukua nafasi ya Kamishna Wambura aliyeteuliwa juzi na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkurugenzi Upelelezi na  Makosa ya Jinai (DCI).

Msemaji wa polisi nchini, David Misime alisema leo Jumatatu Mei 31, 2021 kuwa Sirro amefanya mabadiliko hayo madogo ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi na Kamishna Wambura pamoja na Kamishna Hamad Khamis Hamad aliyeteuliwa na Rais Samia kuwa Kamishna wa Kamisheni ya Fedha na Logistiki.

Katika mabadiliko hayo, Sirro amemhamisha Naibu Kamishna wa Polisi (DCP), Lucas Mkondya kutoka kuwa Kaimu Kamishna wa Fedha na Logistiki makao makuu ya Polisi Dodoma kuwa Mkuu wa Usalama Barabarani Tanzania (Trafiki).

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rufiji, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Onesmo Lyanga,  amehamishwa kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, akichukua nafasi ya Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Gilles Muroto ambaye anastaafu.

Mabadiliko hayo yalimgusa pia Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Ramadhan Ngh’anzi akihamishwa kutoka kuwa Boharia Mkuu kwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa  Mwanza. Kamanda Ngh’anzi aliwahi kuwa kamanda wa polisi wa Arusha.

“Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), Mwamini Rwantale amehamishwa kutoka Kanda Maalum ya Dar es Salaam ambako alikuwa Mkuu wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu na sasa anakuwa Kamanda wa Polisi Kikosi cha Tazara,” alisema Sirro kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari.

Sirro amefafanua kuwa aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Polisi Tazara, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Stella Richard amepelekwa kuwa  Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida.

Pia Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Zuberi Chambera amehamishwa kutoka makao makuu ya upelelezi Dodoma,  kwenda makao makuu ya polisi Zanzibar akishika nafasi ya Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa Jinai visiwani humo.

Related Articles

Back to top button