Habari

INEC yatangaza siku 65 uboreshaji daftari la kudumu la wapiga kura awamu ya pili

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza siku 65 za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya pili, utakaofanyika kuanzia Mei Mosi hadi Julai 4, 2025, utakaoenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura.

Akizungumza na vyombo vya habari jana Jumatatu Aprili 14 jijini Dodoma, Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufani, Jacobs Mwambegele, amesema uboreshaji wa daftari utafanyika kwa mizunguko mitatu.

Jaji Mwambegele amefafanua kuwa, mzunguko wa kwanza wa uboreshaji huo utajumuisha mikoa 15, wakati mzunguko wa pili ukihusisha mikao 16 na mzunguko wa tatu utajumuisha Vituo vya Magereza na Vyuo vya Mafunzo.

Ameitaja mikoa itakayohusika kwenye mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kuwa ni pamoja na Geita, Kagera, Mara, Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Rukwa, Tabora, Katavi, Kigoma, Iringa, Ruvuma, Mbeya, Njombe na Songwe, ambapo zoezi hilo litafanyika kuanzia Mei 1 hadi Mei 7, 2025.

Mikoa ya mzunguko wa pili ni pamoja na Arusha, Manyara, Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Pwani, Singida, Dodoma, Dar es Salaam, Lindi, Mtwara, Mjini Magharibi, Kaskazini Unguja, Kusini Unguja, Kaskazini Pemba na Kusini Pemba, uboreshaji huo utafanyika kati ya Mei 16 na 22, 2025.

“Mzunguko wa tatu wa zoezi la uboreshaji wa Daftari utahusisha vituo 130 vilivyopo kwenye Magereza ya Tanzania Bara na vituo 10 vilivyopo katika Vyuo vya Mafunzo Tanzania Zanzibar kwa wakati mmoja na utafanyika kwa muda wa siku saba kuanzia Juni 28 hadi Julai 4, 2025,” amesema Jaji Mwambegele.

Ameongeza kuwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa awamu ya pili, utafanyika ngazi ya Kata kwa Tanzania Bara na ngazi ya Jimbo kwa Tanzania Zanzibar, ambapo jumla ya vituo 7,869 vitahusika, kati ya hivyo, vituo 7,659 vipo Tanzania Bara na vituo 210 vipo Tanzania Zanzibar.

“Tunatarajia kuwa katika awamu ya pili ya uboreshaji, wapiga kura wapya 1,396,609 wataandikishwa, wapiga kura 1,092,383 wataboresha taarifa zao na wapiga kura 148,624 watafutwa kwenye Daftari kwa kukosa sifa za kuendelea kuwepo kwenye Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.

Amesema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa masharti ya kifungu cha 16(5) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya mwaka 2024 kinachoipa Tume jukumu la kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili mara baada ya Uchaguzi Mkuu na kabla ya uteuzi wa wagombea kwa Uchaguzi Mkuu unaofuata.

Wakati huohuo, Jaji Mwambegele amesema kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 11(1) na (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, Tume pia ina jukumu la kuandaa Daftari la Awali la Wapiga Kura na kuliweka wazi kwa umma.

Tume iliboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura awamu ya kwanza kuanzia Julai 20 mwaka jana 2024 na kukamilisha Machi 25 mwaka huu 2025.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents