
Mahakama ya Shirikisho katika Jiji la Chicago Nchini Marekani, Jumatatu wiki hii imeamuru Jiji la Chicago liwalipe dola milioni 120 ambazo ni zaidi ya Bilioni 316 Tsh. ( dola milini 60 kila mmoja) Wanaume wawili ambao ni John Fulton na Anthony Mitchell ambao walihukumiwa kimakosa mwaka 2003 wakidaiwa kumuua Kijana wa miaka 18.
Wakati Mahakama ikiwahukumu kwenda jela wawili hawa, John alikuwa na umri wa miaka 18 huku Anthony akiwa na umri wa miaka 17 ambapo walituhumiwa kumuua Kijana Christoper Collazo aliyekuwa na umri wa miaka 18 wakati huo ambaye mwili wake uligunduliwa katika uchochoro nyuma ya yadi ukiwa umefungwa kwa mkanda na kuchomwa moto kidogo ambapo kesi hiyo iliwafanya wawili hawa kukaa gerezani kwa miaka 16 kabla ya kuachiwa huru mwaka 2019.
Imeelezwa kuwa wawili hawa walipatikana na hatia ya mauaji ya daraja la kwanza na utekaji nyara mwaka 2006 na kuhukumiwa kifungo cha miaka 31 jela lakini waliachiwa mwaka 2019 baada ya Hakimu wa Kaunti ya Cook kufuta mashtaka yao ambapo ilibainika hakukuwa na ushahidi wa kimaumbile uliowahusisha wawili hao na kifo cha Collazo lakini iliwabidi wakiri na kutoa ushahidi wa uongo kwakuwa Polisi waliwatesa kimwili na kisaikolojia.
Hata hivyo Mawakili wa Jiji la Chicago wamesema wanapanga kukata rufaa dhidi ya uamuuzi huu wa Mahakama ya Shirikisho.