Habari

Jamii yatakiwa kuwawezesha wanasayansi chipukizi

Katika hatua ya kukuza na kuendeleza ubunifu wa kisayansi kwa vijana wa shuleni, Taasisi ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST) imeitaka jamii kuwaunga mkono vijana wanaochipukia kwenye sayansi ili waweze kufikia ndoto zao.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa Sayansi katika Shule ya Sekondari Kibaha, Mwalimu Julius Ngasa wakati wa hafla ya kutembelea mradi wa kisayansi ulioendelezwa na wanafunzi wa kidato cha sita wa shule hiyo.

Amesema kuwa sayansi ni nyenzo muhimu sana katika kuchochea ukuaji wa uchumi lakini pia inarahishisha upatikanaji wa ajira kwa vijana wengi wenye malengo ya kufika mbali na hivyo kupunguza utegemezi katika nchi.

Amesema jamii inapoona vijana wenye hari na udhubutu wa kuisaidia jamii yao na kuchochea maendeleo ya nchi kupitia sayansi haina budi kuwashika mkono na kuwawezesha kwa hali na mali ili waweze kufika mbali na kufanikiwa kwenye malengo yao.

“Nashauri wazazi na wadau wa maendeleo wenye nia ya kusaidia maendeleo ya vijana wafanye hivyo ili kuendeleza vipaji vya vijana wanaochipukia,” amesema Mwalimu Ngasa.

Hafla hiyo iliambatana na uwasilishwaji wa taarifa ya mradi wa kisayansi uliobuniwa na Adiani Andrea na Erick Kweyunga ambao ni Wanafunzi wa Kibaha Sekondari uliohusu utumiaji wa mifumo ya kidijiti katika kuwawezesha vijana kupata mwongozo mzuri wa namna ya kujiunga na elimu ya juu ya vyuo vikuu nchini.

Ubunifu wa mradi huu ni sehemu ya jitihada za wadau ikiwemo kampuni ya Shell Tanzania katika kuunga mkono ubunifu wa kisayansi kwa vijana walio wengi nchini.

Akizungumza mara baada ya uwasilishwaji wa taarifa ya mradi, Mshauri Masuala ya Kijamii kutoka Kampuni ya Shell Tanzania Msomisi Mmbena amesema Kampuni hiyo ya Shell Tanzania inaamini katika kuendeleza vipaji vya sayansi kwa kuendeleza vijana wenye ubunifu wanaoweza kutumia sayansi kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

“Shell Tanzania ni kampuni ambayo inauhitaji mkubwa wa vijana wenye vipaji vya kisayansi na ubunifu watakaoweza kutumiwa kuchochea maendeleo ya viwanda kwa kutumia teknolojia,” amesema Mmbena.

Mradi huu wa Aidan na Erick ni sehemu ya maandalizi ya uwasilishwaji wa miradi mingi ya kisayansi ya wanafunzi inayotarajiwa kushindanishwa na miradi ya wanafunzi wa shule nyingine nchini mnamo mwezi wa tisa.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents