Habari

Japan, Marekani zatoa tahadhari ya kutokea kwa Tsunami

Japan na Marekani zimewataka watu wanaoishi kwenye mwambao wa bahari ya Pasifiki kuelekea sehemu za miinuko, kutokana na kitisho cha tsunami baada mripuko wa volkano ya chini ya bahari karibu na kisiwa cha Tonga.

Picha za satelaiti zimeonyesha mripuko wa volkano hiyo ya Hunga Tonga-Hunga Ha’apai, ambao umerusha angani moshi na majivu katika umbo la uyoga mkubwa, na kusababisha tetemeko katika eneo la bahari ya Pasifiki linalokizunguka kisiwa cha Tonga.

Taarifa za taasisi ya hali ya hewa ya Australia zinasema mawimbi yenye kima cha mita 1.2 yalishuhudiwa katika mji mkuu wa Tonga wa Nuku’alofa.

Japan pia imeripoti kuwa mawimbi yaliyotokana na tsunami hiyo yamefika kwenye pwani yake, yakiwa na kima cha hadi mita tatu.

 Watu wahaha wakitafuta sehemu za miinuko    

Hali hiyo imesababisha taharuki na watu wa kisiwa kidogo cha Tonga walionekana wakikimbia mbio kuhamia kwenye maeneo ya vilima.

Infografik Karte Tonga ENAlama ya buluu kwenye ramani inaonyesha ilipo volkano iliyoripuka na kusababisha tsunami

Mmoja wao, Mere Taufa amesema wakati volkano iliporipuka alikuwa nyumbani akijiandaa kwa mlo wa mchana, na aligutushwa na mawimbi ya bahari yaliyoanza kuivamia nyumba yake.

”Lilikuwa tetemeko kubwa sana lililoitikisa ardhi. Kaka yangu alidhani ni mabomu yaliyokuwa yakiripuliwa karibu na nyumba yetu,” alisema Taufa akizungumza na tovuti ya Stuff News.

Mkazi huyo amesema nyumba yao ilifurika maji katika muda wa dakika chache, na kuongeza kuwa aliuona ukuta wa nyumba ya jirani yake ukiporomoka.

”Bila kukawia tulijua kuwa ni tsunami imetokea, kwa kiwango cha maji yaliyoivamia nyumba yetu. Ungeweza kuwasikia watu wakipiga mayowe kila mahali, wakikimbilia maeneo salama, kila mmoja akitafuta sehemu iliyoinuka.”

Muungurumo mithili ya mabomu na radi

Mripuko huo wa volkano ya chini ya bahari ulidumu kwa takribani dakika nane, na umekuja muda mfupi baada ya kutolewa kwa tahadhari ya tsunami nyingine.

Tsunami nach Erdbeben in der SüdseePicha hii ya maktaba inaonyesha pwani ya Samoa baada ya tsunami ya Septemba 2009

Kulingana na duru kutoka mji wa Suva, mripuko huo ulisikika kama miungurumo ya radi katika kisiwa cha Fiji kilicho umbali wa kilomita 800 kutoka kitovu chake, na mawimbi makubwa yaliipiga pwani ya kisiwa hicho.

Miito ya tahadhari imetolewa pia New Zealand, American Samoa, Vanuatu, Chile na Australia.

Onyo la tsunami lilitolewa pia kwa watu waishio pwani ya magharibi ya Marekani, kuanzia California hadi Alaska.

Katika tangazo lake, kitengo cha Marekani cha tahadhari dhidi ya Tsunami kimewaonya watu wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na kitisho, kikisema ”tsunami inakuja, na kumbukeni kuwa mawimbi ya mwanzo hayaonekani makubwa sana. Ondoka kwenye mwambao muhamie kwenye miinuko.”

Canada pia imetoa angalizo kama hilo kwa watu wa mkoa wa British Columbia, ikiwaasa kuepuka kwenda ufukweni.

Source: Deutsche Welle

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents