
Jay-Z amshitaki mwanamke ambaye mwezi Februari aliondoa kesi yake ambayo alimtuhumu mwanamuziki huyo kwa ubakaji.
Katika kesi yake hiyo ya kukashifiwa, anadai mwanamke huyo “alikiri kwa hiari” kwamba alishinikizwa kutoa madai ya uwongo katika “njama” ya kujipatia pesa na kuharibu sifa yake.
Mwanamke huyo ambaye jina lake halijuulikana aliwasilisha kesi yake ya kisheria mwezi Oktoba na kuifungua tena mwezi Disemba, akimshutumu Jay-Z, ambaye jina halisi ni Shawn Carter, na Sean “Diddy” Combs kwa kumbaka akiwa na umri wa miaka 13, baada ya tuzo za MTV Video Music Awards za 2000.
Wanamuziki wote wawili walikanusha madai hayo.
Kesi ya Jay-Z, iliyowasilishwa katika mahakama ya shirikisho huko Alabama, pia inamshtaki wakili wa mwanamke huyo, Tony Buzbee, na wakili mwenzake, David Fortney, kwa kuandaa kesi ya mwanamke huyo.
Bw Buzbee ni wakili wa makumi ya kesi alizowasilisha kwa niaba ya watu wanaomtuhumu Bw Combs kwa unyanyasaji wa kingono, unyang’anyi, unyanyasaji mwingine.
Combs amekanusha tuhuma zote.
Katika kesi ya Jay-Z, wanasheria hao wanasema mwanamke huyo ameiambia timu hiyo, kuwa wanasheria wake walimfanya atoe madai hayo ya uwongo.
Katika kesi ya Jay-Z, timu yake ya wanasheria inasema kampuni ya Buzbee ilishindwa kukagua madai ya mwanamke huyo, ambaye wanasema ana historia ya matatizo ya afya ya akili.
Buzbee amekana kufanya makosa yoyote na anadai timu ya Jay-Z ilimtisha mwanamke huyo ili abatilishe taarifa zake.
Jay- Z, ambaye ni mume wa Beyoncé, anasema shutuma hizo zimesababisha madhara kwake binafsi na kazi yake, ikiwa ni pamoja na kupoteza kandarasi za biashara zenye thamani ya takriban dola za kimarekani milioni 20 (£15.8m) kwa mwaka katika kampuni yake, Roc Nation, na kuiathiri familia yake, hasa watoto wake.