Jeraha la Kidunda lasababisha pambano lake dhidi ya Katompa wa DRC kusitishwa
Jeraha alilolipata bondia Selemani Kidunda katika raundi ya tatu limesababisha kumalizwa bila mshindi katika pambano la kusaka ubingwa wa IBF dhidi ya bondia kutoka DRC Katompa.
Kidunda alichanika juu ya paji lake la uso baada ya kugongwa na kichwa cha Katompa jambo lililomsababishia kushindwa kuendelea na pambano hilo kutokana na kuvuja damu nyingi kwasababu ya jeraha kuwa kubwa.
Kwamujibu wa msimamizi wa mkanda huo ni kuwa bondia Selemani Kidunda angeweza kupewa ushindi endapo pambano hilo lingefika raundi ya nne kwani jerahi alilolipata lilitokana na kuchezewa mchezo usio wa kiungwana kwa makusudi na mpinzani wake aliyetumia kichwa kumjeruhi lakini sheria za IBF zinawalazimu kutoa matokeo ya sare kwasababu tu tatizo hilo limejitokeza katika raundi ya tatu.
Hata hivyo upande wa Bondia Katompa amelalamikia uamuzi wa kumaliza pambano hilo akiamini mpinzani wake angeweza kuendelea na mchezo huo baada ya kupatiwa matibabu
Bondia Kidunda yeye amemlaumu Katompa kwa kumsababishia jeraha hilo kwa makusudi na kusema kuwa amemchafulia rekodi yake kwani hajawahi kutoka sare katika mapambano yake.
Pambano hilo lilikuwa la raundi kumi.