
Jeshi la Israel linasema linapanga mashambulizi ya ardhini, angani na baharini – lakini hatujui ni lini mashambulizi ya ardhini yanayotarajiwa yataanza.
Jumamosi jioni, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitembelea wanajeshi waliokuwa wakijiandaa kwa shambulizi hilo.
Picha za video zilimuonyesha akiwa amevalia fulana ya kuzuia risasi akiongea na wanajeshi waliokuwa na silaha nzito katika makazi ambayo yalikuwa yakilengwa na wanamgambo wa Hamas katika shambulio la Jumamosi iliyopita, walipojipenyeza Israel.
“Uko tayari kwa kile kinachokuja? Mengi zaidi yanakuja,” anasema kwenye video.
Mashambulizi makali ya anga ya Israel yaliendelea usiku kucha. Mamilioni ya watu wa Gaza wametakiwa kuhama kaskazini mwa eneo hilo – huku wengi wakitoroka kwa gari au kwa miguu.