Jeshi la Polisi lapiga marufuku maandamano ya Chadema
Jeshi la Polisi limepiga marufuku maandamano yaliyopangwa kufanywa na chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Septemba 23, 2024 jijini Dar es Salaam.
Taarifa ya marufuku hiyo imetolewa na Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime akielezea kuwa kufanya hivyo ni kuingilia hatua za kiupelelezi zinazoendelea kuhusu matukio mbalimbali ya mauaji na utekaji.
“Jeshi la Polisi nchini linatoa onyo kwa viongozi wa chama hicho, kuacha kuendelea kuhamasisha wananchi kujihusisha katika uhalifu huo, na yeyote atakayeingia barabarani atakabiliwa vilivyo kwa mujibu wa sheria za nchi, kwa maana hiyo maandamano hayo yamepigwa marufuku”
“Jeshi la Polisi linatoa katazo kwa yeyote aliyealikwa, kuelekezwa kufika Dar es Salaam kutoka mkoa wowote ule kwa ajili ya maandamano hayo asithubutu kufanya hivyo, kwani maandamano hayo ni haramu na hayatafanyika” amesema.
Aidha Misime ametoa rai kwa wananchi kutokubali kurubuniwa, kudanganywa au kushawishiwa kwa namna yoyote ile kushiriki katika maandamano hayo na badala yake waendelee kushirikiana na jeshi la polisi kutoa taarifa ya viashiria vyovyote vya uvunjifu wa Amani.
Written by Janeth Jovin