Habari

Jeshi, raia kujadili kuundwa kwa serikali ya mpito Guinea

Utawala wa kijeshi nchini Guinea unatazamiwa kukumbana na shinikizo la kutangaza ratiba ya uchaguzi mpya wakati ukianza mikutano ya siku nne juu ya mustakbali wa taifa hilo la Afrika Magharibi.

Wasiwasi unazidi kuongezeka juu ya namna baraza hilo la kijeshi linaloongozwa na Kanali Mamady Doumbuya litakavyorejesha serikali ya mpito ya kiraia kama walivyotakiwa na wapatanishi wa kikanda na jumuiya ya kimataifa.

Mapinduzi yenyewe ya wiki iliyopita yalipokelewa kwa tahadhari na wapinzani wa muda mrefu wa Rais Alpha Conde, akiwemo kiongozi mkuu wa upinzani, Cellou Dalein Diallo, ambaye alishawania na kushindwa mara tatu kwenye uchaguzi.

Hasira juu ya uamuzi wa Conde kuwania muhula wa tatu mwaka jana zilipelekea maandamano ya umma mitaani, na watu wengi katika mji mkuu, Conakry, wameonesha kuliunga mkono jeshi kwa uamuzi wake wa kutwaa madaraka.

Lakini kudumu kwa uungaji mkono huu unategemea zaidi na jinsi mikutano ya wiki hii itakavyofanikisha kufikia makubaliano kati ya jeshi na makundi ya kiraia.

Washiriki wa mikutano ya utawala wa mpito

Cellou Dalein DialloKiongozi mkuu wa upinzani wa Guinea, Cellou Dalein Diallo, asema atashiriki uchaguzi kama ukiitishwa upya.

Miongoni mwa wanaoshiriki kwenye mikutano huyo ni viongozi wa sekta ya madini, ambao baraza la kijeshi linataka kuwahakikishia usalama wao ili kuzuwia kusambaratika kwa usafirishaji wa dhahabu na madini mengine muhimu unaoushikilia uchumi wa nchi hiyo.

Lakini kwa kuanzia, hivi leo watawala wa kijeshi wanakutana na viongozi wa chama kikuu cha upinzani, Union of Democratic Forces of Guinea, kinachoongozwa na Diallo, na wakosoaji wengine wa Conde.

Baadaye wanajeshi hao watakutakana na viongozi wa kidini katika jengo liitwalo Kasri la Umma, ambako awali walilitumia kuwaita maafisa wa serikali iliyopinduliwa na kuwataka wakabidhishe hati zao za kusafiria na magari ya serikali waliyokuwa wakiyatumia.

Umoja wa Mataifa wataka umma uamuwe

Guinea ECOWAS-Delegation in Conakry Wajumbe wa ECOWAS wakiwa mjini Conakry kusaka suluhisho la kisiasa baada ya mapinduzi ya kijeshi.

Baada ya ziara yake mjini Conakry jana Jumatatu, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika Magharibi na Ukanda wa Sahel, Annadif Khatir Mahamat Saleh, alisema anaweka matumaini yake makubwa kwenye mikutano ya wiki hii.

“Kwa sababu chochote jumuiya ya kimataifa itakachosema ama kufanya, hatima ya Guinea ni kile Waguinea wenyewe watakachoamuwa,” alisema mjumbe huyo maalum.

Diallo ameweka wazi kwamba atawania tena urais ikiwa uchaguzi mpya utaitishwa. Kwenye mahojiano yake na shirika la habari la AP Jumapili iliyopita, kiongozi huyo wa upinzani na aliyewahi kuwa waziri mkuu wa Guinea, alimuita Conde kuwa ni dikteta aliyejitafutia mwenyewe balaa lililomfika kwa kukataa kwake kuheshimu ukomo wa mihula ya urais kama ilivyowekwa kikatiba.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya Afrika ya Magharibi (ECOWAS) tayari imeshatishia kuiwekea vikwazo Guinea ikiwa utawala wa kijeshi haukumuachilia huru rais huyo aliyepinduliwa, hatua ambayo iliichukuwa pia mwaka jana pale mapinduzi ya kijeshi yalipofanyika nchini Mali.

Related Articles

Back to top button