Ofisi ya AG yapendekeza Julai Mosi kuanza kutumika kwa toleo la sheria zilizofanyiwa urekebu

Na Mwandishi wetu, Dodoma
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Hamza Johari amesema kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imependekeza Julai Mosi, 2025 iwe ni tarehe ya kuanza kutumika kwa toleo la sheria zilizofanyiwa urekebu la mwaka2023.
Johari ameyasema hayo leo Aprili 23, 2025 wakati wa hafla ya uzinduzi wa Toleo la Sheria zilizofanyiwa urekebu la mwaka 2023 iliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.
Amesema pendekezo la tarehe hiyo ni ili kutoa fursa ya usambazaji wa sheria hizo kabla ya tarehe ya kuanza kutumika na kwamba ameeleza kuwa baada ya tarehe hiyo toleo hilo litaanza kutumika kama sheria halali na sahihi za nchi na litatambuliwa na mahakama zote na mamlaka zingine kama rejea sahihi ya sheria zilizofanyiwa urekebu.
Hata hivyo Johari amesema urekebu wa sheria ni mradi walioufanya uliolengo kufanya majumuisho ya marekebisho ya sheria mbalimbali yanayofanywa na Bunge kuwa kitu kimoja ili kurahisisha upatikanaji, usomwaji na utumiaji wa sheria hizo.
Amesisitiza kuwa hiyo ni kazi ya msingi inayolenga kuboresha na kurahisisha matumizi ya sheria za nchi na kwa kufanya hivyo wanahakikisha sheria za nchi zinabaki kuwa hai zinazoendana na wakati na zinaeleweka kwa urahisi na wananchi.
“Zoezi hili limehusisha kusasisha (Update) sheria zetu kwa kujumuisha marekebisho yaliyofanyika tangu toleo la mwisho la mwaka 2002, kurekebisha makosa ya kiuchapaji na kuziweka sheria hizo katika mfumo unaoeleweka vizuri.
Toleo la urekebu utakalolizindua leo Mh Rais limejumuisha sheria Kuu 446 ambazo zimegawanywa katika juzuu zipatazo 21, zipo sheria mpya 171 zilizotungwa Kati ya mwaka 2002 na 2023,” amesema Johari
Aidha Johari amesema toleo hilo ni zao la kazi ya miaka minne kwa maana mwaka 2020 hadi 2024 na limefanikishwa kwa kutumia rasilimali za ndani chini ya Serikali ya awamu ya sita na kwamba hiyo imeweka historia kwani ni tofauti na toleo la mwaka 2002 lililofadhiliwa na Benki ya Dunia.
“Kutokana na haya Serikali yako Mh Rais inadhihilisha uwezo wa ndani kwa vitendo, hii inaashiria dhamira ya kweli ya kujitegemea na kuwekeza katika mifumo Imara ya kisheria kwa maendeleo ya Taifa letu,” amesema
Aidha amesema kumekuwa na mageuzi na jitihada mbalimbali katika usimamizi wa sheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambayo kwa namna moja yamechagiza kukamilika kwa zoezi hilo.
“Mageuzi haya yalijumuisha kuongeza nguvu kazi kwa kuajili zaidi ya mawakili wa serikali 50, na kuanzisha Ofisi ya Mwendesha Mkuu wa Sheria, jitihada hizi chini ya uongozi wako Rais Samia ni ishara tosha kuwa serikali yako inayoongoza inakusudia kuendelea kuboresha utendaji kazi katika sekta ya sheria,” amesema
Hata hivyo amesema wakati wakitekekeza mradi huo wa urekebu wa sheria walibaini kuwa baadhi ya maboresho yanahitaji kufanyika kwa njia ya marekebisho ya sheria ya Bunge hivyo Wizara ya Katiba na Sheria iliandaa muswada kwa ajili ya kutungwa kwa Sheria kwa ajili ya marekebisho ya Sheria mbalimbali yaliyotokana na zoezi hili la urekebu.
Written by Janeth Jovin