Habari

Jomo Kenyatta airport kukodishwa kwa miaka 30 wafanyakazi wagoma

Shughuli katika uwanja mkuu wa ndege wa Kenya zilitatizika baada ya wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kuanzisha mgomo Jumanne usiku wakipinga mapendekezo ya kukodisha uwanja huo kwa miaka 30 kwa kampuni ya Adani ya India.

Shirika la ndege la Kenya Airways limetoa taarifa kuelezea kutatizika kwa shughuli zake.

‘’Kwa sababu ya hatua zilizochukuliwa na wafanyakazi wa shirika la JKIA, hili limesababisha kuchelewa na hata kuahirishwa kwa baadhi ya safari za ndege zinazoingia na zinazotoka’’.

Muungano wa wafanyikazi wa sekta hiyo ulikuwa umeonya kuhusu mgomo usiojulikana baada ya serikali kukosa kufichua maelezo ya mpango huo tata.

Foleni ndefu zilishuhudiwa huku mamia ya wasafiri waliokwama wakisubiri, na kuathiri shughuli za ndege katika uwanja wa ndege wenye shughuli nyingi zaidi Afrika Mashariki.

Picha kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha idadi kubwa ya abiria wakijaribu kuchukua mizigo yao katika uwanja wa JKIA huku mgomo huo ukianza kuamkia Jumatano.

Serikali ilisema kuwa mpango huo, unaojumuisha ujenzi wa njia ya pili ya ndege na kituo kipya, uko kwenye mkataba wa kampuni hiyo ya kibinafsi kujenga na kisha kuanza kuusimamia kwa kipindi cha miaka kadhaa.

Pia ilifafanua kuwa bado hakuna uamuzi uliotolewa, lakini ukiidhinishwa, utatekelezwa ili kulinda maslahi ya taifa la nchi.

Siku ya Jumanne, Mahakama Kuu ilizuia kwa muda mpango huo.

Chama cha Wanasheria nchini Kenya na Tume ya Haki za Kibinadamu ziliwasilisha ombi, zikisema kuwa mpango huo haukuwa wa lazima, kwani Kenya inaweza kukusanya dola bilioni 1.8 zinazohitajika kuboresha uwanja huo wa ndege.

Walionya kuwa kukodisha uwanja huo kunaweza kusababisha upotezaji wa kazi na ukosefu wa thamani kwa walipa kodi.

Chama cha upinzani nchini India cha Congress pia kilikosoa mpango huo, kikidai kuwa unaweza kuongeza uhasama dhidi ya maslahi ya Wahindi nchini Kenya.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents