Jukwaa la Panda Digital lenye lengo la kuwajengea uwezo Wasichana lazinduliwa Dar (Video)

hirika la Her Initiative kwa kushirikiana na kampuni ya Serengeti Bytes limezindua jukwaa la kidigitali la kwanza la kiswahili lenye lengo la kuwasaidia wasichana kupata ujuzi na rasilimali za kuanza na kuendesha biashara zao ili kufikia malengo ya kujikwamua kiuchumi.

Jukwaa hili linafahamika kama Panda Digital likiwa na maana ya kupanda mbegu ya kujitegemea kiuchumi kwa kupitia majukwaa ya kidigitali. Jukwaa hili linawaleta pamoja wasichana wajasiriamali popote walipo Tanzania na kuwajengea uwezo pamoja na kuwapa ujuzi wa masuala mtambuka wa biashara na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za ufadhili, mitaji na mikopo zilizopo katika taasisi binafsi na za serikali.

Jukwaa la Panda digital limeanzishwa kwa lengo la kuwajengea uwezo na kuwapatia wasichana ujuzi utakaowasaidia kutengeza kipato kwa kuanzisha na kuendesha biashara, kuchochea ushiriki wa wanawake vijana katika uchumi wa kidigitali, kuwaunganisha wasichana na fursa za kifedha kama mitaji, mikopo, ufadhili, kuhamasisha uvumbuzi na ubunifu miongoni mwa wasichana na kuhakikisha wasichana wana uhakika wa kuongeza ujuzi wa kukabiliana na changamoto kibiashara hasa katika kipindi cha majanga kama COVID 19.
Vilevile jukwaa la Panda Digital linatarajiwa kuwa kanzidata maalumu ya wasichana na wanawake wajasiriamali kutoka mikoa yote ya Tanzania.
Pia, Panda Digital itakuwa jukwaa la wasichana wajasiriamali kutangaza bidhaa na/au huduma zao kupitia kipengele maalumu kinachofahamika kama Soko.

Katika jukwaa hili kutakuwa na kozi mbalimbali za kuongeza ujuzi wa kibiashara kama kozi za masoko mtandaoni, huduma kwa wateja, namna ya kutengeneza chapa ya biashara na namna ya kufanya ufungashaji na masuala mengine kama namna ya kukabiliana na changamoto za kibiashara. Kwa sasa kozi iliyokamilika ni kozi ya masoko mtandaoni na tayari imewekwa kwenye jukwaa la Panda Digital kwa ajili ya matumizi. Kozi ya masoko mtandaoni ina masomo 12 na sehemu ya maswali na majibu iliyoambatanishwa kila baada ya kumaliza somo moja lengo ni kuwasaidia wajasiriamali kupata uelewa zaidi.

Related Articles

Back to top button