Habari

Kaburi la Baba mzazi wa Spika Ndugai lafukuliwa

Ikiwa ni miaka 25 tangu Yustine Ndugai ambaye ni baba mzazi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai azikwe katika Kitongoji cha Katente mkoani Geita, kaburi lake limefukuliwa na mabaki yake kuchukuliwa na ndugu zake ili kwenda kuzikwa upya katika Kijiji cha Ibagwe, wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Tokeo la picha la Job Ndugai
Spika wa Bunge, Job Ndugai

Mabaki ya mzee huyo aliyefariki dunia Mei 22, 1992 yalichukuliwa na wanaukoo juzi wakiongozwa na Spika Ndugai.

Mwenyekiti wa umoja wa wazee kitongoji cha Katente Namba Moja, Joseph Kitafuma alisema walimpokea mzee huyo kijijini hapo kama mchimbaji mdogo wa dhahabu mwaka 1986. Kitafuma alimuomba Spika Ndugai kuwajengea zahanati kwani aliyotibiwa baba yake wakati anaugua imechakaa sana na kusema zahanati hiyo itapewa jina la Ndugai, ombi ambalo kiongozi huyo wa bunge alilikubali.

Mbunge wa Bukombe, Dotto Biteko aliwataka wananchi kuona umuhimu wa kuwatunza wazazi na kuhamisha makaburi yao kwa kufuata mila na desturi za eneo husika. Alisema kuwa, kitendo kilichofanywa na spika ni cha kuigwa kwani kinaonyesha anatambua umuhimu wa wazazi si tu wakiwa hai lakini pia baada ya kufariki dunia.

“Sitasahau wema na utu walioonyesha wananchi wa Bukombe kutunza kaburi la baba yangu kwa miaka 25,” alisema Spika Ndugai huku akimtaka Mkuu wa Wilaya, Mbunge na Mkurugenzi wa Halmashauri kusimamia ujenzi wa zahanati kama walivyooomba wazee wa kijiji hicho.

Ufukuaji wa mabaki hayo ulifanyika baada ya kupata idhini ya mahakama.

Chanzo: Mwananchi

Posted by Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents