Kamanda wa kwanza wa kike wa NASA: ”Sikutaka waseme ‘mwanamke amefanya kosa”

Yeye ndiye mwanaanga za juu aliyevuka vikwazo na akaendelea mbele bila kusita.
Eileen Collins aliandika historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuendesha na kuongoza chombo cha angani. Licha ya mafanikio yake ya kipekee, bado si watu wengi wanaojua jina lake.
Sasa, filamu ya maisha yake iitwayo Spacewoman, inayosimulia safari yake ya kipekee na mafanikio yake makubwa, inalenga kuibadilisha hali hiyo.
Tunamkuta Collins katika chumba cha Makumbusho ya Sayansi, jijini London.

Ni mtu mpole, mwenye mvuto wa kirafiki na unyenyekevu wa hali ya juu. Lakini si muda mrefu kabla hujagundua msimamo wake thabiti na malengo yake yaliyo wazi. Anaonekana kuwa na nguvu ya ndani isiyoyumba.
“Nilikuwa nasoma makala kwenye jarida kuhusu wanaanga wa Gemini. Nadhani nilikuwa na umri wa takribani miaka tisa, na nikajisemea, ‘Hicho ndicho ninachotaka kufanya’,” anasema.
“Bila shaka, wakati huo hakukuwa na wanawake wanaanga. Lakini nikawaza, ‘Nitakuwa mwanaanga wa kike.'”
Lakini ndoto yake haikuishia hapo alitamani zaidi. Alitaka kuwa rubani na kuwa nyuma ya usukani wa chombo cha anga.
Njia pekee ya kufanikisha hilo ilikuwa kujiunga na jeshi na kuwa rubani wa majaribio.
Katika Jeshi la Anga, aliibuka na kuwa mmoja wa waliochaguliwa kujiunga na mpango wa wanaanga wa NASA, ambapo alipewa nafasi ya kurusha ndege za anga za Space Shuttle, chombo cha angani kilichoweza kutumika zaidi ya mara moja.
Alijua macho ya dunia yalikuwa juu yake wakati wa safari yake ya kwanza mnamo 1995.
“Kama mwanamke wa kwanza kuendesha Space Shuttle, nilifanya kazi kwa bidii sana kwa sababu sikutaka watu waseme, ‘Tazama, mwanamke amefanya kosa’. Kwa sababu haikuhusu mimi tu ilikuwa kuhusu wanawake wengine watakaokuja baada yangu,” anasema.
“Nilitaka wanawake rubani wajulikane kwa ubora wao: watu waseme, ‘Hawa ni wazuri sana’.”

Na kwa kweli, alikuwa bora kiasi kwamba aliteuliwa kuwa kamanda wa safari ya angani hatua nyingine ya kihistoria.
Mbali na kazi yake ya kihistoria, Collins pia alikuwa mama wa watoto wawili wadogo. Ukweli kwamba alikuwa mke, mama, na mwanaanga wa NASA ulizua mshangao katika mikutano ya waandishi wa habari.
Wengine walishindwa kuamini kwamba aliweza kubeba majukumu yote hayo kwa wakati mmoja.
Lakini Collins anasema kuwa mama na kuwa kamanda ni “kazi mbili bora kabisa duniani.”
“Lakini ukweli ni kwamba ni vigumu zaidi kuwa mzazi kuliko kuwa kamanda wa Space Shuttle,” anasema kwa kucheka.
“Mafunzo bora kabisa niliyowahi kupata kwa ajili ya kuwa kamanda yalitokana na kuwa mzazi kwa sababu unalazimika kujifunza kusema ‘hapana’.”

Safari za Space Shuttle, zilizodumu kwa zaidi ya miaka thelathini, zilileta mafanikio makubwa lakini pia ziligubikwa na misiba mikubwa.
Mnamo mwaka 1986, chombo cha Challenger kililipuka sekunde chache baada ya kurushwa, na kuua wanaanga wote saba waliokuwemo.
Mnamo 2003, Columbia kilivunjika hewani juu ya anga la Texas wakati kikirejea kutoka angani, na kusababisha vifo vya wanaanga saba pia.
Chanzo kilikuwa ni kipande cha povu kilichojitenga kutoka kwenye tanki la mafuta wakati wa kurushwa, kikaharibu kinga ya joto ya chombo hicho. Columbia haikuweza kustahimili moto mkali wa kuingia tena kwenye anga la dunia, na kiliteketea kabisa huku ulimwengu ukiangalia kwa huzuni.
Collins anakumbuka tukio hilo kwa maumivu kwani alipoteza marafiki wa karibu.
Lakini kama kamanda, alilazimika kuendelea. Safari iliyofuata ilikua chini ya uongozi wake.

Je, alifikiria kuachana na safari hiyo?
“Watu wengi waliokuwa ndani ya mradi wa Space Shuttle walitegemea kuwa kamanda ataendelea,” anasema kwa sauti ya utulivu.
“Kuacha kungekuwa kinyume na ujasiri… Nilitaka kuwa kiongozi mwenye ujasiri, mwenye kujiamini na niwe chanzo cha imani kwa wengine.”
Kwa mikono imara kwenye usukani na sauti ya utulivu akiwa kwenye mawasiliano na kikosi cha mpango kazi cha misheni hiyo, Collins aligeuza chombo hicho kwa mzunguko wa taratibu na wenye ustadi mkubwa. Picha zilizoonyesha upande wa chini wa chombo zilisaidia kugundua uharibifu mapema na matembezi ya angani yalifanyika ili kufanya marekebisho.
Collins na timu yake walirudi salama nyumbani.

Hiyo ilikuwa safari yake ya mwisho. Anasema alikusudia kumaliza kazi yake baada ya misheni ya nne ili kuwapa wengine nafasi ya kwenda anga za juu.
Ameshuhudia wanaanga wengi wakifuata nyayo zake. Je, ana ushauri kwa kizazi kijacho kinachoota kufika kwenye nyota?
“Fanya kazi zako za shule, msikilize mwalimu wako, zingatia darasani, na soma vitabu. Hiyo itakupa msingi mzuri wa kujenga ndoto zako,” anasema kwa wepesi.
cc: BBC Swahili






