Kamati ya siasa yakagua miradi ya Bilioni Tano Nyasa

Kamati ya siasa ya Mkoa wa Ruvuma ikiongozwa na Mwenyekiti wake Komredi Odo Mwisho, imetembelea na kukagua Miradi ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi Bilioni tano katika Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa, mkoani Ruvuma na kuagiza utekelezaji wake ukamilike kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.
Akiongoza ukaguzi wa Kamati ya Siasa ya Mkoa katika Kata ya Chiwanda, Mwisho alikagua miradi ya zaidi ya Sh milioni 622 ikiwemo mabweni mawili (Sh milioni 256), bwalo la chakula (Sh milioni 61) katika Shule ya Sekondari Nyasa na ujenzi wa Kituo cha Afya Chiwanda cha Sh milioni 250.
Aidha, Kupitia mpango wa BOOST, Shule ya Msingi Chimate pia inanufaika na mradi wa Sh milioni 154 wa madarasa, nyumba ya walimu na vyoo. Miradi mingine iliyokaguliwa ni pamoja na shule mpya Limbo (Sh milioni 314), madarasa Ndesule (Sh milioni 72), jengo la akina mama Mbambabay (Sh milioni 23.8) na mradi mkubwa wa maji Nangombo wa Sh bilioni 3.78.

Vilevile, Mwisho amesisitiza kuwe na uwazi kwa wananchi kuhusu fedha za miradi zinazotolewa na watekelzaji wake wajulikane na kuwataka watendaji kusimamia kikamilifu utekelezaji wake.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mhe. Peres Magiri, ameitaka halmashauri kuhakikisha wakandarasi wanalipwa kwa wakati ili miradi ikamilike na kuanza kuhudumia wananchi.
Naye, Mjumbe kamati kuu, Dkt Sharif Ngonyani, amewaomba Wakandarasi kuwa na moyo wa kujitoa kwa manufaa ya wananchi, huku akisisitiza malipo yao kufanyika kwa wakati ili kuendelea kuwatia moyo watendaji hao kuendelea kufanya kazi kwa ubora na kwa wakati.
Serikali kupitia awamu ya sita, imefikia kufanya ukaguzi huo ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi wa Nyasa.
Written by Angel Kayombo







