Habari

Kapinga awataka watanzania kutokuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa umeme

Azindua namba ya bure ya huduma kwa mteja

NAIBU Waziri wa Nishati, Judith Kapinga amewataka Watanzania wasiwe na hofu wala wasiwasi kuhusu upatikanaji wa nishati ya umeme kwa sababu serikali imejipanga na iko makini.

Kapinga ameyaeleza hayo leo Machi 12,2025 wakati akizindua namba mpya ya huduma kwa wateja ya TANESCO ya 180  bila gharama katika Kituo cha miito ya simu mkoani Dar es Salaam.

Amesema Serikali imedhamiria na imejipanga kuhakikisha Watanzania wanapata huduma bora ya umeme na ya uhakika kwa wakati wote kupitia Tanesco.

Waziri Kapinga amefafanua kuwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeweka lengo la kuwahudumia Watanzania wapate huduma bora ya umeme ikiwamo umeme wa uhakika kwa wakati wote.

“Hivyo niwaombe Watanzania wasiwe na wasiwasi wala hofu juu ya upatikanaji wa umeme hapa nchini, tutaendelea kuboresha mazingira na miundombinu yetu,” amesema

Kuhusu uzinduzi wa namba hiyo, Waziri Kapinga amesema awali Watanzania walikuwa wanatozwa fedha walipokuwa wanapiga ili kupata huduma lakini kwa sasa ni bure.

Amesema kituo cha miito ya simu uwezo wake ni  kupokea simu za huduma kwa wateja 15,000 kwa siku, lakini hadi kufikia Julai mwaka jana kituo hicho kilipokea simu 50,000.

Hatua ya kuboresha huduma ya simu kwa wateja ilitokana na agizo la Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko alipofanya ziara mwaka jana katika kituo hicho na kutoa maagizo ya maboresho.

“Wizara ya Nishati itaendelea kuzisimamia sekta zilizochini yake ikiwemo TANESCO na REA ili kuhakikisha huduma bora ya umeme inapatikana na kuwafikia Watanzania wote. Pia Wizara itakuwa kinara katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Waziri Kapinga.

Kadhalika, Waziri Kapinga ametoa maagizo matano, Kwanza aliwataka wapokea simu za wateja kuzingatia weredi na kutoa kauli njema na kuhudumia wateja kwa wakati.

Pili, aliwataja mameneja wa TANESCO mikoa wapokee kero za Watanzania na kuzitatua ndani ya saa 24 kama ilivyopangwa, tatu ni Watanzania waendelee kutumia umeme nafuu kupitia majiko ya TANESCO.

Nne, aliwataka uongozi wa TANESCO kukisimamia vizuri kituo cha miito ya simu kwa wateja na kuhakikisha inatoa adhabu kali kwa wahudumu watakao kichafua kituo hicho.

Tano, aliwataka Watanzania kituo cha miito ya simu kwa uweledi na uangalifu ili wenye shida  za kweli waweze kuhudumiwa kwa wakati.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO, Gisima Nyamohanga amesema kituo hicho kitatumika kuwasiliana  na wateja wao na kwamba mteja hatatumia namba hiyo bila gharama yoyote.

, “Kituo hiki kinatumika kuwasiliana na wateja wetu. Awali wateja wetu walipokuwa na tatizo na kutupigia walikuwa wanalipia lakini leo tumetekeleza agizo la Naibu Waziri Mkuu la kuweka namba ya bure”. Amesema

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents