Kesi ya Nicole yashindwa kuendelea kutoka na upelelezi kutokamilika

Kesi ya kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu, kuanzisha magrupu ya kuchezesha biashara ya upatu kinyume na sheria inayomkabili, msanii Joyce Mbaga maarufu kama Nicole imeshindwa kuendelea kutokana na upelelezi wake kutokamilika.
Mbali na Nicole (32) mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Rehema Mahanhu ambapo kwa pamoja walifikishwa mahakamani hapo Machi 10, 2025 na kusomewa mashtaka yao na Wakili wa Serikali, Rhoda Maingu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ramadhan Rugemalira.
Katika kesi hiyo iliyotajwa leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, upande wa Jamhuri umeieleza mahakama kwamba upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo wanaomba ahirisho ili waendelee kukamilisha upelelezi.
Hata hivyo kutokana na maombi hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi April 14, 2025.
Nicole na Manhu wapo nje kwa dhamana, ambapo walifikishwa mahakamani hapo wakikabiliwa na mashtaka matatu ikiwemo kuongoza genge la uhalifu wakituhumiwa kuendesha biashara ya kihalifu au jinai, kwa lengo la kujipatia faida kutoka kwa jamii na kupokea amana au miamala bila kupata leseni kutoka BOT.
Katika shtaka la pili washtakiwa wote wanatuhumiwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025 wakiwa eneo lisilofahamika ndani ya mkoa wa Dar es Salaam walipokea amana ya Sh 185,515,000 kutoka kwa jamii bila kuwa na leseni.
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la tatu washtakiwa waliendesha mfumo wa malipo bila kuwa na leseni ya malipo inayotolewa na BoT.
Written by Janeth Jovin




