Kikao cha Maafisa Utamaduni na Michezo

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Gerson Msigwa amesema kuwa Washiriki zaidi ya 900 wamehudhuria Kikao kazi cha Maafisa Utamaduni na Maafisa Maendeleo ya Michezo Tanzania wakijadili mambo mambo mbalimbali juu ya kuleta mabadiliko katika sekta hizo.
Msigwa ameyasema hayo Aprili 22, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akitoa utambulisho na maelezo mafupi kwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.
Aidha Msigwa amesema kuwa, miongoni mwa mafanikio ya kikao hicho ni kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili maafisa hao katika utekelezaji wa majukumu ikiwemo upungufu wa rasilimali watu.
“Kutoka mwaka 2021 hadi mwaka 2025 Idadi ya wataalamu wa utamaduni wameongezeka kutoka 43 hadi 123 na idadi ya wataalamu wa michezo kutoka 48 hadi 139” alieleza Msigwa.
Kikao kazi hicho kinafanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere kuanzia Aprili 22 na kitatamatika Aprili 25, 2025.