Kiongozi wa Kimila Akemea Taarifa za Uwongo Mitandaoni

Kiongozi wa kimila nchini Tanzania, Dkt. Fadhili, ametoa wito kwa vyombo vya habari na watumiaji wa mitandao ya kijamii kuacha kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho ambazo zinaweza kuleta taharuki kwa jamii.
Akizungumza kuhusu tukio lililosambaa hivi karibuni la madai ya watu kuibiwa sehemu zao za siri (nyeti), Dkt. Fadhili amesema taarifa hizo si za kweli na zimekuwa zikichochewa na baadhi ya watu wachache kwa maslahi yao binafsi.
Amesisitiza kuwa kwa mujibu wa taarifa alizozipokea kutoka kwa msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, hakuna tukio lolote lililoripotiwa kuthibitisha madai hayo. Aidha, alifafanua kuwa watu waliodai kuibiwa nyeti walipofikishwa kwa ajili ya uchunguzi na ukaguzi, walibainika kuwa hawakuwa na tatizo hilo, hali inayodhihirisha kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote.
Dkt. Fadhili amesisitiza umuhimu wa vyombo vya habari kufuata maadili ya taaluma kwa kuhakikisha wanachapisha habari zilizothibitishwa ili kulinda amani na utulivu wa jamii.
Kwa upande wake, ametoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizo na kuendelea na shughuli zao za kila siku bila hofu, huku akiwahimiza kupata taarifa sahihi kutoka kwenye vyanzo vinavyoaminika.




