Habari

Kitabu cha hayati Mwalimu Nyerere kuingia kwenye mitaala ya vyuo Indonesia

KATIKA kusherehekea miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Indonesia, Ubalozi wa Indonesia nchini Tanzania umezindua vitabu viwili vyenye lengo la kukuza lugha za mataifa hayo mawili.

Kitabu kimoja kilichozinduliwa ni kile kilichoandikwa na Rais wa Indonesia, Joko Widodo na kingine ni cha hayati Mwalimu Julius Nyerere ambavyo vimetafsiriwa kwa lugha ya kiswahili na Kiindonesia (Kibahasa) ili viweze kutumika kwenye mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na vyuo vikuu kama sehemu ya kukuza matumizi ya lugha hizo kwa mataifa hayo.

Uzinduzi wa vitabu hivyo umefanyika jijini Dar es Salaam katika hafla ya kusherehekea miaka 79 ya Jamhuri ya Indonesia sambamba na kusherehekea miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na indonesia, ulioanza mwaka 1964 n kuendelea kuimarika kila wakati.

Akizungumza katika sherehe hizo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Dennis Londo aliipongeza Jamhuri ya Indonesia kwa kutimiza miaka 79 ya Uhuru huku wakiendelea kuenzi yale yaliyoazimiwa Agosti 17, 1945 wakati wa uhuru wa ]nchi hiyo.

Alisema uwepo wa vitabu hivyo unatoa fursa kwa watu hasa wanafunzi kuweza kujisomea na kuelewa kwa kina historia ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Balozi wa Indonesia nchini Tanzania, Tri Yogo Jatmiko, alisema kitabu cha Mwalimu Nyerere cha Our Leadership and Destiny of Tanzania kimetafsiriwa kuwa ‘Kepemimpinan Kami Dan Takdir Tanzania, huku kitabu cha Jokowi and the New Indonesia kikitafsiriwa kuwa ‘Jokowi Ametimiza Ndoto za Indonesia’.

Alisema anaishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano wake wa dhati, akibainisha kuwa sekta kama biashara na elimu zimeimarisha zaidi uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa hayo mawili na kubainisha kuwa Indonesia imejidhatiti kuendeleza na kuimarisha uhusiano huo kwa manufaa ya pande zote mbili.

Sherehe hizo zilihudhuriwa pia na mabalozi na wawakilishi wa nchi mbalimbali, Wizara, Taasisi na Mashirika mbalimbali akiwemo pia aliyekuwa Waziri wa Mambo ya nje, Liberata Mulamula.

Mwezi Agosti mwaka jana, Widodo (Jokowi) wa Indonesia alifanya ziara Tanzania iliyofuatiwa na ziara ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan nchini Indonesia mwaka huu.

Ziara hizo zimesaidia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi katika sekta za biashara, uwekezaji, nishati, kilimo, madini, uchumi wa buluu, elimu, kati ya mengine mengi.

Written by Janeth Jovin

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents