Michezo

Kocha asiyeona, anavyojipanga kutamba soka la Tanzania

“Watu hawaamini kama nina uwezo wa kufundisha soka kwasababu tu siwezi kuona. Hilo linanipa wakati mgumu japo kama mwalimu wa mpira wa miguu inanipa nafasi ya kujiamini zaidi,” anaeleza Kocha wa timu ya Mfaranyaki City, Priver Ngonyani.

Sasa fika uwanjani uyaone maajabu…

BBC ilifika katika uwanja wa Mfaranyaki uliopo wilayani Songea, kusini mwa Tanzania.

Sauti za wachezaji zilisikika, milio ikiwa mingi vijana wakipiga pasi za mpira, huku wakifuata maelekezo madhubuti kutoka kwa kocha wao.

Lakini katika hali ambayo wengi hawajaizoea tunashuhudia kocha Priver akifanya yake pembezoni mwa uwanja.

Sasa kocha huyo ana ulemavu wa macho, lakini anaamini kuwa masikio yake ni kama macho. Anaweza kusikia kila hatua ya wachezaji wake, kila mguso wa mpira, na kila nafasi inayojitokeza uwanjani.

Mara nyingi anaonekana akisikiliza kwa makini huku akili yake ikibeba ramani ya uwanja licha ya kutouona mpira kwa macho yake.

Anasema anaweza kutambua nani anacheza vizuri na nani hajafanikisha majukumu yake.

“Sioni lakini masikio yangu husikia vyema na hisia zina nguvu kubwa sana za kunisaidia. Hii inanifanya nijue huyu anacheza vizuri au huyu mwingine anacheza vibaya,” anasema kocha Priver.

Nini kilimsukuma kufundisha soka?

Kocha huyo anasema, “Kwa kuona vijana wengi wanakaa mtaani na kujishughulisha na shughuli ambazo si nzuri kama uvutaji sigara, matumizi ya pombe niliona nitafute kitu cha kufanya ambacho kitasaidia kuwaepusha wengi kutoka kwenye mambo ambayo si mema.”

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 27 aliyezaliwa na ulemavu wa macho anasema licha ya kuwa wengi hutazama soka kwa macho yao, yeye huelewa kila kitu uwanjani kupitia masikio na hisia.

Anasema alipenda kusikiliza uchambuzi wa soka redioni, na huko alijifunza mengi ikiwemo mbinu mbalimbali za soka.

Alipotangaza azma ya kuwa kocha, anasema wengi walimcheka. “Kocha gani haoni?” walihoji. Lakini kwa Priver, changamoto ya kutokuona haikuwa sababu ya yeye kushindwa kutimiza malengo yake.

Kocha huyo ni mwandishi wa habari kitaalama lakini hajawahi kuajiriwa katika chombo chochote cha habari.

Anasema, “Nilisoma diploma ya uandishi wa habari na mpaka sasa, miaka imeenda sijapata ajira. Sasa wengine hawatuamini sisi walemavu, hata kama utampelekea kitu hakuamini au kuonesha unaweza pia hakuamini…

“…binafsi mimi changamoto nyingi nakabiliana nazo kama sehemu ya maisha,” anasema Priver.

Mpaka sasa ni miaka 10, kocha Ngonyani anaendelea kujitolea kuvinoa vikosi vya wachezaji 46 wa timu ya Mfaranyaki City FC. Kati yao 24 wanaunda kikosi cha wakubwa na wengine ni vijana wa timu ya U20, U17, na U14.

Nidhamu kwake kipaumbele

Licha ya changamoto zake, wachezaji wa timu hiyo waliieleza BBC kuwa wanamheshimu na kufuata maelekezo ya kocha huyo kwa umakini.

Benedict Mindi, ambaye kocha msaidizi wa timu ya Mfaranyaki City FC anasema,” Tumepata mafanikio makubwa kwa miaka miwili sasa nikiwa msaidizi wake. Daima yuko tayari kufanya maamuzi na wakati mwingine anakataa mabadiliko ikiwa anaona hayafai. Ameleta nidhamu na mafanikio makubwa ndani ya timu.”

Naye nahodha wa timu hiyo, Rogatus Mbawala anasema kuwa wanafuata maagizo ya kocha na kwamba hawatumii ulemavu wake kama sababu ya kupuuza maagizo yake.

Unyanyapaa bado changamoto kwenye jamii

g

Nje ya uwanja, Ngonyani anasema kuwa anakumbana na changamoto nyingi.

Tanzania, kama ilivyo kwa mataifa mengine, watu wenye ulemavu wanakumbwa na vikwazo vya kijamii na kiuchumi.

Kwa mujibu wa Shirika la kimataifa la kukabiliana na ulemavu wa macho linaeleza kuwa kuna watanzania 290,000 vipofu nchini Tanzania.

Ngonyani anasema soka limempa jukwaa la kuthibitisha kuwa uwezo haupimwi kwa macho, bali kwa akili na moyo.

“Wachezaji wangu wananiamini na kufuata mwongozo wangu. Wanaponiona, hawaoni kipofu bali wanaona kocha na mimi ni kocha kama wengine,” anasema kocha huyo.

‘Kilimo kinaendesha timu hiyo’

Priver anasema timu yake inakabiliwa na changamoto za kifedha, mara nyingi hutegemea michango ya watu binafsi ili kujiendesha.

“Ili kupata vifaa vya mazoezi, tunajitahidi kukusanya pesa sisi wenyewe kwa wenyewe. Wakati mwingine tunafanya kazi kwenye mashamba ya watu ili kupata fedha za kununua mipira na jezi,” anasema Ngonyani.

Wazazi wajivunia

Licha ya changamoto hizo, baba yake Priver, Titus Ngonyani anajivunia mafanikio ya mwanawe.

Ngonyani anasema, “Watu wanamshangaa Priver alivyo na anavyofanya. Umaarufu wake ameupata kwa kuwafundisha soka na hikoni kipaji cha kipekee ambacho sisi tunajivunia.”

Ndoto zake

Ngonyani ana ndoto ya kufundisha timu kubwa nchini Tanzania hapo badae.

“Kama wakinipa nafasi na sapoti basi mtaona nikifanya makubwa na ni dhahabu ambayo wengi hawaioni ila ipo siku watakuja kuona umuhimu wa mimi hapo mbele,” anasema Ngonyani.

Kwa upande wake, Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tanzania (TFF) limesema kuwa limekuwa likitoa sapoti kwa watu wenye ulemavu kufanikisha ndoto zao kwenye kisoka.

TFF imekuwa na utaratibu wa kutoa mafunzo kwa makocha na kutoa msaada wa vifaa kwa timu za wanaume na wanawake wenye ulemavu wa viungo.

Mkurugenzi wa Ufundi wa shirikisho hilo, Oscar Mirambo anasema,”Tuko tayari kusaidia mtu yoyote, akiwemo kocha huyo kwani mpira wa miguu ni mchezo wa kila mtu.”

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents