Kama Bodi ya Ligi Kuu Tanzania na idara ya ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) watasimamia vyema kanuni za Ligi Kuu msimu huu, hakuna namna Kocha mpya wa Yanga, Hamdi Miloud atalazimika kushushwa cheo na kuwa kocha msaidizi kwa daraja lake la leseni halitoshi kumfanya awe kocha Mkuu wa timu inayoshiriki Ligi Kuu ya NBC na badala yake anapaswa kuwa msaidizi.
.
Yanga ilianika hadharani wasifu wake ambao ulionyesha kuwa Mualgeria huyo ana leseni daraja A iliyotolewa na Umoja wa Vyama vya Mpira wa Miguu Ulaya (Uefa).
.
Kanuni ya 77 ya Ligi Kuu imefafanua sifa za kocha mojawapo ikiwa ni hadhi ya leseni inayofafanua kuwa kocha mwenye leseni kutoka nje ya Afrika anapaswa kuwa na ngazi ya Pro Diploma ambayo kwa Afrika ni sawa na Diploma daraja A.
.
3.1 “Kocha mkuu wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau Pro Diploma au inayolingana nayo. 3.2 Kocha msaidizi wa klabu ya Ligi Kuu kutoka nje ya bara la Afrika anatakiwa kuwa na angalau A Diploma au inayolingana nayo.
.
“Kocha wa timu ya Ligi Kuu kutoka nje ya Tanzania ni lazima awe amefundisha klabu ya Ligi Kuu au timu ya Taifa katika nchi yoyote ndani ya kipindi cha miaka miwili iliyopita,” inafafanua kanuni hiyo
.
Wakati kanuni zikimbana Miloud, kocha msaidizi Abdihamid Moalin yeye ana sifa stahiki za kuliongoza benchi la ufundi la Yanga kwa vile ana leseni daraja A inayotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika.