Korea Kaskazini yafyatua makombora mawili ya masafa marefu

Korea Kaskazini imefyatua makombora mawili ya masafa marefu kutoka pwani ya mashariki ya taifa hilo , jeshi la Korea Kusini limethibitisha.

Japan pia iliripoti kwamba kuna kitu kilichofyatuliwa kuelekea angani ambacho inahisi huenda ni kombora la masafa mrefu.

Waziri mkuu wa Japan Yoshihide Suga amelitaja jaribio hilo la kombora kama la kikatili akisema linatishia usalama na amani ya eneo hilo.

Ni jaribio la pili la silaha kufanywa wiki hii, huku la kwanza likiwa kombora la masafa mafupi.

Haijulikani ni wapi makombora hayo yalianguka, lakini mkuu mwenza wa majeshi nchini Korea kusini amesema kwamba jeshi la taifa hilo limejiandaa vilivyo likishirikiana kwa karibu na lile la Marekani.

Majaribio ya silaha za masafa marefu yanakiuka maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kuzuia mpango wa kinyuklia ya taifa la Korea kaskazini.

Silaha hizo zinaweza kubeba vichwa vya kinyuklia na huorodheshwa kulingana na umbali ambao yanaweza kufika – huku kombora linalosafiri umbali zaidi likiwa lile linaloweza kuruka kutoka bara moja hadi jingine kwa jina (ICBM).

Korea kaskazini awali imefanikiwa kufanyia majaribio kombora la ICBM ambalo linadaiwa kuwa na uwezo wa kufika magharibi mwa Ulaya na nusu ya bara la Marekani.

Siku ya Jumatatu, Korea kaskazini ilifanyia majaribio kombora la masafa mafupi lililodaiwa kuwa na uwezo wa kushambulia eneo kubwa la Japan , likitaja kombora hilo kama lile la kimkakati na lenye umuhimu mkubwa.

Related Articles

Back to top button