Kwaya ya Flying Family yavutiwa na utulivu, maajabu ya Ziwa Duluti

Januari 9, 2026, Kwaya ya Flying Family (FFC) ilifanya ziara maalum ya kutembelea Ziwa Duluti, moja ya vivutio vya kipekee vya utalii wa ikolojia kilichopo kaskazini mwa Tanzania, ndani ya Jiji la Arusha.
Ziwa Duluti, ingawa ni dogo kwa ukubwa, linatajwa kuwa na maajabu makubwa yanayolifanya kuwa kivutio muhimu cha utalii wa asili. Ziwa hilo limejaa siri na mvuto unaowavutia wageni wa ndani na nje ya nchi kulitembelea na kujionea uzuri wake wa kipekee.
Kupitia ziara hiyo, wanakwaya wa FFC walielezwa kuwa Ziwa Duluti liliundwa na mlipuko wa volkano wa zamani, hali inayolipa umbo la duara pamoja na kina kirefu. Ziwa hilo lipo katika mazingira ya utulivu mkubwa, likizungukwa na misitu ya asili, jambo linalolifanya kuwa eneo bora kwa mapumziko na tafakari ya kina.
Akizungumza na wanakwaya hao, mmoja wa waongoza watalii alisema kuwa kivutio kikubwa zaidi katika Ziwa Duluti ni kisiwa kinachohama kwa upepo.
Alieleza kuwa kisiwa hicho kimeundwa na mimea, matope pamoja na mizizi iliyosokotana, hivyo hakijashikamana moja kwa moja na sakafu ya ziwa. Aliongeza kuwa upepo unapovuma, kisiwa hicho husogea taratibu kutoka upande mmoja wa ziwa hadi mwingine, tukio linalowaacha wageni wengi midomo wazi kwa mshangao.
“Maji ya Ziwa Duluti ni tulivu na yana rangi ya kijani inayodhihirisha kina chake kikubwa. Ukimya wa ziwa hili huvunjwa na sauti za ndege wa porini wanaolizunguka, hali inayolifanya eneo hili kuwa mahali sahihi kwa wapenda mazingira, wapiga picha na wale wanaotafuta utulivu wa kiakili,” amesema mwongozaji huyo wa watalii.
Ameongeza kuwa Ziwa Duluti ni makazi ya aina mbalimbali za ndege wa majini, samaki na viumbe wengine wa asili. Wageni wanaotembelea ziwa hilo hupata fursa ya kushiriki shughuli mbalimbali ikiwemo kupanda mtumbwi, matembezi ya asili (nature walk), utazamaji wa ndege pamoja na kupiga picha za mandhari.
Kwa kuzingatia mazingira yake ya asili, amesema Ziwa Duluti lina nafasi kubwa ya kukuza utalii endelevu, likiwa kivutio kinachofaa kwa familia, wanandoa, wanafunzi pamoja na watalii wanaotaka kujifunza na kufurahia maajabu ya asili bila kuharibu mazingira.
Kwa upande wake, Febronia Tesha, ambaye ni mwanakwaya wa sauti ya pili katika kwaya ya Flying Family, amesema amefurahia ziara hiyo kwani imemwezesha kujifunza na kujionea mambo mbalimbali ambayo hapo awali hakuwahi kuyafahamu.
“Hakika Ziwa Duluti linaonesha uzuri na utajiri wa Tanzania. Ukiwa hapa unapata nafasi ya kutafakari mambo mengi. Nitoe wito kwa wananchi na wageni wengine kuja kulitembelea na kujionea kwa macho yao kisiwa kinachohama kwa upepo,” amesema Tesha
Written by Janeth Jovin










